Michezo

Juventus waingia fainali ya Coppa Italia licha ya Ronaldo kupoteza penalti

June 13th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 13 wa taji la Coppa Italia, Juventus, walitinga fainali ya kipute hicho msimu huu kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya AC Milan kwenye mkondo wa pili jijini Turin.

Baada ya kusajili sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliosakatiwa mjini Milan mnamo Februari 13, Juventus walishindwa kuliona lango la wageni wao katika marudiano ya nusu-fainali yaliyowakutanisha ugani Allianz bila mashabiki.

Nyota Cristiano Ronaldo alipoteza mkwaju wa penalti katika kipindi cha kwanza kabla ya Ante Rebic wa Milan kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 16.

Adhabu dhidi ya Rebic ambaye ni mzawa wa Croatia, ilikuwa zao la yeye kumkabili vibaya beki wa Juventus, Danilo Luiz da Silva, 28.

Chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Maurizio Sarri, Juventus kwa sasa watakutana na mshindi kati ya Inter Milan na Napoli kwenye fainali itakayoandaliwa jijini Roma mnamo Jumatano ya Juni 17, 2020.

Napoli watajitosa ugani leo Jumamosi ya Juni 13, 2020, kuvaana na Inter huku wakijivunia ushindi wa 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Baada ya wachezaji wote wa Juventus na Milan kuingia uwanjani, kulikuwapo na kimya cha dakika moja kwa heshima ya watu ambao wameangamia kutokana na homa kali ya corona hadi kufikia sasa, kisha maafisa wa usalama wanaojitahidi kukabiliana na janga hilo la dunia wakapigiwa makofi.

Kukosekana kwa mashabiki uwanjani kulifanya mchuano huo kuonekana kama kipindi kingine chochote cha mazoezi kati ya wanasoka wa kikosi kimoja wanaofahamiana. Ingawa hivyo, kasi ya mechi ilibadilika baada ya wenyeji kupewa penalti iliyopotezwa na Ronaldo.

Juventus walipewa penalti hiyo baada ya marejeleo ya video ya teknolojia ya VAR kubainisha kuwa mchezaji mmoja wa Milan alikuwa ameunawa mpira ndani ya kijisanduku chao.

Kombora la Ronaldo liligonga mhimili wa goli la Milan dakika chache kabla ya Rebic kufurushwa uwanjani.

Ingawa kupungua kwa idadi ya wachezaji wa Milan kuliwapa Juventus hamasa zaidi ya kulivamia lango la wageni wao, kipa Gianluigi Donnatumma alifanya kazi ya ziada na kuyapangua mashuti aliyoelekezewa na Ronaldo, Blaise Matuidi na Paulo Dybala.

AC Milan ambao kwa sasa wana alama 27 nyuma ya Juventus wanaoselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa pointi 63, walikosa huduma za mshambuliaji wao mkongwe, Zlatan Ibrahimovic anayeuguza jeraha la mguu.

Soka ya Italia iliyosimamishwa mnamo Machi 9 kutokana na corona zikiwa zimesalia mechi 12, imepangiwa kurejea Juni 20 huku pengo la alama moja pekee likitamalaki kati ya Juventus na Lazio wanaokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Serie A.