Michezo

Juventus wajinasia maarifa ya fowadi matata Federico Chiesa kutoka Fiorentina

October 6th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wamemsajili fowadi Federico Chiesa kutoka Fiorentina kwa mkataba ambao unakisiwa kuwa wa Sh7.6 bilioni.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 anaingia katika sajili rasmi ya Juventus kwa mkopo wa miaka miwili kabla ya kupokezwa mkataba wa kudumu.

Chiesa alipokezwa malezi ya soka kambini mwa Fiorentina kabla ya kuwajibishwa kwa mara ya kwanza dhidi ya Juventus mnamo 2016.

Baada ya mechi hiyo, aliwajibishwa na Fiorentina katika zaidi ya mechi 150 na akapata fursa ya kuchezea timu ya taifa ya Italia mara 19.

Enrico ambaye ni baba ya Chiesa, aliwahi kuchezea Parma kwa pamoja na kipa wa sasa wa Juventus, Gianluigi Buffon katika miaka ya 1990.

Maafikiano ya kumshawishi Chiesa kutua jijini Turin yatashuhudia Juventus wakilipa Fiorentina Sh1.4 bilioni za mwanzo kwa misimu miwili kabla ya kuweka mezani Sh4.4 bilioni nyinginezo ili kufanikisha uhamisho wake kwa mkataba wa kudumu ambao kwa pamoja na ada nyinginezo fiche, utafikia Sh7.6 bilioni.

Beki Mattia de Sciglio pia amebanduka kambini mwa Juventus na kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Olympique Lyon ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kwa mkopo wa mwaka mmoja.