Juventus wajinyanyua ligini na kupepeta limbukeni Salernitana 2-0

Juventus wajinyanyua ligini na kupepeta limbukeni Salernitana 2-0

Na MASHIRIKA

JUVENTUS waliweka kando maruerue ya kupoteza mechi mbili mfululizo ligini na kuwapokeza Salernitana kichapo cha 2-0 ugenini mnamo Jumanne usiku.

Wenyeji Salernitana ambao kwa sasa wanavuta mkia wa jedwali la Serie A wanashiriki kipute hicho msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 1999. Juventus waliwateremkai wakilenga kujinyanyua siku chache baada ya Chelsea kuwapiga 4-0 kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nao Atalanta kuwacharaza 1-0 ligini.

Paulo Dybala alifungulia Juventus ukurasa wa mabao kabla ya Giorgio Chiellini kushuhudia goli lake likifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR.

Alvaro Morata alijaza kimiani bao la pili la Juventus naye Dybala akipoteza mkwaju wa penalti.

Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 24 sawa na nambari sita Fiorentina. Ni pengo la pointi 11 ndilo linawatenganisha na viongozi Napoli.

Kwingineko, nambari nne Atalanta wakichabanga Venezia 4-0 huku Fiorentina wakitandika Sampdoria 3-1.

Dusan Vlahovic alipachika wavuni bao lake la 39 la Serie A akichezea Fiorentina katika mechi hiyo. Erling Braut Haaland ndiye mwanasoka wa pekee aliyezaliwa katika miaka ya 2000 ambaye anajivunia kufunga mabao zaidi miongoni mwa ligi kuu tano za bara Ulaya.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Siku ya Ukimwi Duniani: Vijana washauriwa wawe mstari wa...

Viongozi wa kanisa warudishia mbunge pesa alizochangisha

T L