Juventus wakabwa koo na Verona katika Serie A

Juventus wakabwa koo na Verona katika Serie A

Na MASHIRIKA

JUVENTUS walilazimishiwa na Hellas Verona sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyowakutanisha uwanjani Marcantonio Bentegodi mnamo Februari 27, 2021.

Matokeo hayo ya Juventus yaliwasaza katika nafasi ya tatu kwa alama 46, saba nyuma ya viongozi Inter Milan wanaotiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus walitangulia kuona lango la wenyeji wao katika dakika ya 49 baada ya kukamilisha krosi ya kiungo Federico Chiesa. Goli hilo lilikuwa la 19 kwa Ronaldo kufunga hadi kufikia sasa msimu huu.

Juhudi za Ronaldo zilifutwa na Antonin Barak aliyesawazishia Verona katika dakika ya 77 baada ya kujaza kimiani krosi aliyopokezwa na Darko Lazovic.

Nusura Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A wafungwe mabao mawili zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila kipa Wojciech Szczesny akajituma zaidi na kupangua makombora aliyoelekezewa na Lazovic.

Verona wamewahi kutawazwa mabingwa wa Serie A msimu wa 1984–85.

Inter watafungua pengo la alama 10 kati yao na Juventus iwapo watazamisha chombo cha Genoa katika mechi ya Serie A mnamo Februari 28, 2021.

MATOKEO YA SERIE A (Februari 27):

Verona 1-1 Juventus

Spezia 2-2 Parma

Bologna 2-0 Lazio

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sancho aweka rekodi ya uchangiaji mabao katika soka ya...

Man-City wacharaza West Ham United na kuanza kunusia taji...