Na MASHIRIKA
JUAN Cuadrado alifunga bao na kusaidia Juventus kupepeta Genoa 2-0 katika ushindi uliowapaisha hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Fowadi huyo wa zamani wa Chelsea alipachika wavuni bao kupitia mkwaju wa kona katika dakika ya nane kabla ya mshambuliaji Paulo Dybala kufunga goli la pili katika dakika ya 82. Juventus ya kocha Massimiliano Allegri wangalifunga mabao zaidi katika mchuano huo ila wanasoka wao Matthijs de Ligt na Alvaro Morata wakazidiwa ujanja na kipa Salvatore Sirigu.
Genoa ambao hawakuelekeza kombora lolote langoni mwa Juventus katika vipindi vyote viwili vya mchezo sasa wanashikilia nafasi ya 18 kwa alama 10, moja mbele ya nambari 19 Cagliari na mbele kuzidi limbukeni Salernitana wanaovuta mkia.
Kichapo kutoka kwa Juventus kiliendeleza masaibu ya Genoa ambao sasa hawajafunga bao katika mechi nne ambazo wametandaza hadi kufikia sasa chini ya kocha mpya Andriy Shevchenko.
Juventus kwa sasa wanajivunia alama 27 sawa na Fiorentina. Ni pengo la pointi saba linalotenganisha Juventus na nambari nne Atalanta. Juventus wameshinda mechi tano kati ya sita zilizopita katika mashindano yote.