Michezo

Juventus wanyakua taji la Serie A kwa msimu wa tisa mfululizo

July 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS walitwaa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya tisa mfululizo baada ya kuwapepeta Sampdoria 2-0 jijini Turin mnamo Julai 26, 2020.

Nyota Cristiano Ronaldo aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kupokezwa krosi na Miralem Pjanic anayetazamiwa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona mwishoni mwa msimu huu. Bao hilo la Ronaldo lilikuwa lake la 31 hadi kufikia sasa katika kivumbi cha Serie A.

Goli la pili la Juventus ambao kwa sasa wananolewa na kicha wa zamani wa Chelsea, Maurizio Sarri lilipachikwa wavuni na Federico Bernardeschi katika dakika ya 67.

Juventus ndicho kikosi cha pekee kuwahi kunyanyua ubingwa wa ligi mara tisa mfululizo miongoni mwa vikosi vyote vya Ligi Kuu tano za bara Ulaya yaani Uingereza (EPL), Italia (Serie A), Uhispania (La Liga), Ujerumani (Bundesliga) na Ufaransa (Ligue 1).

Kwa kutia kapuni ufalme wa Serie A muhula huu, Juventus wanaendeleza rekodi yao ambayo Bayern Munich ya Ujerumani ilifikia Juni 2020 baada ya kunyanyua ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya nane mfululizo.

Ronaldo alikosa fursa ya kumfikia na hata kumpiku mfumaji wa Lazio, Ciro Immobile ambaye kwa sasa ni mshindani wake mkuu katika vita vya kupigana taji la Mfungaji Bora wa Serie A muhula huu.

Hii ni baada ya sogora huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid kushuhudia penalti yake mwishoni mwa kipindi cha pili ikibusu mwamba wa goli la Sampdoria.

Immobile ambaye kwa sasa anajivunia mabao 34, anamzidi Ronaldo kwa magoli matatu. Fowadi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Sevilla alipachika wavuni mabao matatu katika ushindi wa 5-1 uliosajiliwa na Lazio dhidi ya Verona katika mechi nyingine ya Julai 26.

Juventus walijibwaga uwanjani wakihitaji kuvuna ushindi mara moja pekee kutokana na mechi tatu walizokuwa wamesalia nazo msimu huu. Hii ni baada ya kupoteza fursa ya kujitwalia taji hilo mnamo Julai 23, 2020 ambapo walipokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Udinese. Mchuano dhidi ya Sampdoria ulikuwa wao wa pili kusajili ushindi kutokana na sita ya awali.

Licha ya kuzamisha chombo cha Sampdoria, mchezo wa Juventus ulikuwa wa kiwango cha chini na ni majaribio yao manane pekee kati ya 19 yaliyolenga shabaha kwenye goli la wageni wao.

Ushindi huo ulimvunia Sarri ambaye pia amewahi kunoa Napoli ya Italia taji lake la kwanza la ligi katika historia ya ukufunzi.

Juventus sasa wanaingia katika kundi moja na Celtic kutoka Scotland na Ludogorets Razgrad kutoka Bulgaria ambao wamewahi kutia kibindoni mataji ya Ligi Kuu za mataifa yao kwa misimu tisa mfululizo.

Rekodi ya dunia kwa kikosi kilichowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara nyingi zaidi inashikiliwa na klabu ya Tafea iliyowahi kunyanyua ufalme wa Ligi Kuu ya Vanuatu kwa misimu 15 mfululizo kati ya 1994 na 2009. Lincoln Red Imps ya Gibraltar na iliyokuwa klabu ya Skonto nchini Latvia zinajivunia rekodi ya bara Ulaya baada ya kutwaa ubingwa wa soka ya mataifa yao kwa mara 14 mfululizo.

Olympique Lyon ya Ufaransa waliwahi kujizolea ubingwa wa Ligue 1 mara saba mfululizo kati ya 2002 na 2008 huku Real Madrid ya Uhispania ikinyanyua ufalme wa La Liga mara tano kwa mpigo, mara mbili zaidi kuliko Huddersfield, Arsenal, Liverpool na Manchester United ambao ni washiriki wa pekee wa EPL kuwahi kutawazwa mabingwa wa soka ya Uingereza mara tatu mfululizo.

Miongoni mwa washiriki wa Ligi Kuu tano za bara Ulaya, Juventus ndio wanaojivunia rekodi ya kunyanyua mataji mengi zaidi ya ligi (36). Wanawapiku mabingwa wapya wa La Liga, Real kwa mataji mawili zaidi.

MATOKEO YA SERIE A (Julai 26, 2020):

Juventus 2-0 Sampdoria

Bologna 3-2 Lecce

Cagliari 0-1 Udinese

Roma 2-1 Fiorentina

Spal 1-1 Torino

Verona 1-5 Lazio