Juventus wapepeta Atalanta na kutwaa ubingwa wa Coppa Italia

Juventus wapepeta Atalanta na kutwaa ubingwa wa Coppa Italia

Na MASHIRIKA

MABAO kutoka kwa Federico Chiesa na Dejan Kulusevski yaliwawezesha Juventus kuwatandika Atalanta 2-1 na kuzoa taji la Coppa Italia mnamo Jumatano.

Kombe hilo ni la kwanza kwa kocha Andrea Pirlo kujizolea katika taaluma yake ya ukufunzi na ni la 14 kwa Juventus kutia kapuni kwenye soka ya Coppa Italia.

Kulusevski aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao katika dakika ya 31, sekunde chache baada ya kushuhudia mpira aliopokezwa na Cristiano Ronaldo ukigonga mwamba wa goli la Atalanta.

Hata hivyo, Ruslan Malinovskyi alisawazishia Atalanta katika dakika ya 41 kabla ya Chiesa kuwarejesha waajiri wake uongozini kunako dakika ya 73.

Atalanta walikamilisha fainali hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki 4,300 ugani Mapei wakiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani baada ya Rafael Toloi kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kuhudhuriwa na mashabiki nchini Italia katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tangu taifa hilo liathiriwe pakubwa na janga la corona.

Juventus ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) wako katika hatari ya kukosa kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao ikizingatiwa kwamba imesalia mechi moja pekee kabla ya kampeni za kipute hicho muhula huu kukamilika rasmi.

Atalanta waliotawazwa mabingwa wa Coppa Italia kwa mara ya mwisho mnamo 1963, sasa wameshindwa katika fainali ya kipute hicho kwa mara ya pili mfululizo baada ya kupigwa na Lazio 2-0 mnamo 2019-20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Aston Villa wadidimiza matumaini ya Spurs kuwa miongoni mwa...

Liverpool wapepeta Burnley na kuingia ndani ya mduara wa...