Habari Mseto

KAA yapiga mnada ndege zilizokawia maegeshoni

January 24th, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) imetangaza mipango ya kupiga mnada ndege 92 zinazomilikiwa na mashirika tofauti ya ndege na watu binafsi, ambazo zimeegeshwa katika viwanja vyake vinne vya ndege kote nchini.

Kupitia tangazo la gazeti la serikali lililochapishwa Ijumaa iliyopita, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KAA Henry Ogoye alitambua ndege 70 katika uwanja wa ndege wa Wilson, 11 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), saba Lokichoggio na ndege nne Malindi ambazo zitapigwa mnada katika muda wa siku 30 zijazo.

Bw Ogoye alisema wahusika walioorodheshwa wanapaswa kuchukua ndege zilizoegeshwa katika viwanja hivyo vya ndege.

Kulingana na Bw Ogoye, tangazo hilo linaandamana na masharti ya Sheria ya Uuzaji Bidhaa Zisizokusanywa, ambayo inawapa mamlaka ya kupiga mnada bidhaa zilizoachwa chini ya masharti fulani.

“Ndege hizo zinakiuka Viwango na Kanuni za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Kanuni za Usalama za Mamlaka ya Usafiri wa Anga (KCAA), ambazo uchukuzi lazima ufanyike ndani ya siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya kuchapishwa kwa notisi hii na baada ya malipo ya gharama zote ambazo hazijalipwa na gharama zozote zinginezo, ikiwa ni pamoja na gharama ya uchapishaji wa notisi hii,” ikasema sehemu ya notisi ya gazeti la serikali.

Notisi hiyo ilitoa maelezo ya kina kuhusu kila ndege, ikiwa ni pamoja na aina, alama za usajili, mmiliki wa mwisho anayejulikana, uwanja wa ndege wa kuhifadhi, na eneo mahususi la kuegesha.

Miongoni mwa mashirika ya ndege ambayo ndege zao ziko chini ya mnada huo ni pamoja na 748 Air Services, Fly540, Fly Sax, National Airways, na African Express.

Nyingine ni Capital Airline, Flight Training Centre, Jetways, Skylink Flight Service, DAC Aviation, Freedom Airline, ACE Air, Wilken Aviation, na Reliance Air Charters Standard Aviation.