Michezo

Kabonyo yatia mfukoni Sh300,000 kwa kushinda Opich Pacho

August 7th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KABONYO Kanyagwal FC ilijozolea tuzo ya washindi ya Sh300, 000 baada ya kucharaza Kolwa Central FC 2-0 katika fainali ya makala ya kwanza ya soka ya Opich Pacho mjini Kisumu mnamo Agosti 5, 2018.

Pinto Onyango na Patrick Opiyo walifungia Kanyagwal mabao hayo muhimu mbele ya mamia ya mashabiki walifika uwanjani Jomo Kenyatta kushuhudia fainali hiyo.

Kolwa iliridhika na zawadi ya Sh200, 000 nayo Kajulu FC, ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu, ikatunukiwa Sh100, 000 baada ya kupepeta Railways FC 2-0 kupitia mabao ya Evans Otieno na Robert Ouko.

Mshambuliaji matata wa Migosi FC, Richard Bebeto aliibuka mfungaji bora, Collins Amuok kutoka Railways akanyakua tuzo ya mchezaji bora naye Benson Okinyi wa Kanyagwal akashinda tuzo ya kipa bora.

Waziri wa Michezo na Utalii wa Kaunti ya Kisumu, Achie Alai alipongeza kampuni ya bia ya Kenya Breweries kwa kudhamini mashindano haya. Aliongeza, “Mashindano haya yamesaidia sana katika kutambua talanta ya soka kutoka mashinani na kuikuza.”

Meneja wa Mauzo wa Kenya Breweries eneo la Kisumu, Thomas Okoth alisisitiza kwamba kampuni hiyo imejitolea kukuza talanta katika michezo kote nchini.