Michezo

Kabras mbioni kusajili vipaji 4 vya maana

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wa Enterprise Cup, Kabras Sugar wamefichua azma ya kusajili wanaraga wanne wa haiba kubwa katika juhudi za kujiandaa kwa msimu wa 2020-21.

Kwa mujibu wa mwenyekiti Philip Jalango, Kabras wanalenga kujinasia huduma za mafowadi watatu na beki mmoja ili kuimarisha kabisa uthabiti wa idara hizo.

“Tumeanza kujipanga kwa muhula ujao kwa matarajio ya kurejea kwa matao ya juu zaidi na kutawala kampeni za raga ya humu nchini,” akasema Jalango kwa kusisitiza kuwa wachezaji watakaosajiliwa ni chipukizi walio na uwezo wa kuwachezea kwa kipindi cha kati ya miaka mitano na 10 ijayo.

Mwanzoni mwa msimu uliopita, Kabras walisajili wanaraga Alfred Orege kutoka Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Walter Okoth aliyeagana na Nakuru RFC.

“Ni wanaraga chipukizi ambao walileta mwamko mpya kikosini na kuinua viwango vya ushindani kiasi kwamba mtihani mkubwa ukawa kwa benchi ya kiufundi kuteua nani wa kuwajibishwa dhidi ya mshindani yupi. Hiyo ni ishara ya ubora wa timu,” akasema Jalango.

Muhula wa uhamisho wa wanaraga wa humu nchini unatarajiwa kufunguliwa rasmi wiki ijayo.

Hadi kipute cha Ligi Kuu ya Kenya Cup kiliposimamishwa kutokana na janga la corona, Kabras ambao walipoteza mechi moja pekee dhidi ya Homeboyz mnamo Disemba 2019, walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 74, tatu zaidi kuliko mabingwa watetezi KCB.

Kabras walijizolea taji lao la kwanza la Kenya Cup mnamo 2016 baada ya kuwazaba Impala Saracens 22-5. Tangu wakati huo, wamezidiwa maarifa na KCB kwenye fainali nne za Kenya Cup mnamo 2015, 2017, 2018 na 2019.

Kwingineko, viongozi wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza la Raga ya Kenya (Championship), Strathmore Leos wanaazimia kusajili wanaraga watano.

Chini ya kocha Louis Kisia, Leos hawajazidiwa maarifa katika mechi yoyote kati ya 16 zilizopita. Walikuwa wameratibiwa kuchuana na mshindi kati ya Northern Suburbs na USIU-A kwenye nusu-fainali ya Championship.