Michezo

Kabras na KCB pazuri kushinda Kenya Cup

April 7th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Msimu wa kawaida wa Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) ulitamatika Jumamosi, huku Nakuru, Mwamba na Impala Saracens zikiungana na Kabras Sugar, KCB na Kenya Harlequin katika awamu ya mwisho ya kuamua mshindi wa msimu 2018-2019.

Wanasukari wa Kabras na wanabenki wa KCB walimaliza katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 74 na 72 mtawalia. Kabras ilimaliza msimu kwa kucharaza Impala Saracens 32-22 nayo KCB ilichapa ‘madeejay’ Homeboyz 10-3.

Timu za Kabras na KCB zilitinga nusu-fainali moja kwa moja kwa kumaliza katika nafasi hizo mbili za kwanza. Harlequin, Nakuru, Mwamba na Impala zilifuatana kutoka nafasi ya tatu hadi sita kwa alama 53, 47, 45 na 45, mtawalia.

Klabu hizi nne zitalimana Aprili 27 kutafuta timu mbili zitakazomenyana na Kabras na KCB katika nusu-fainali mnamo Mei 4.

Fainali ni Mei 11. Mabingwa mara 17 Nondescripts walifungiwa nje ya mduara wa klabu sita-bora kwa kupoteza mechi ya mwisho japo pembamba 15-12 dhidi ya Harlequins.

Walitamatisha msimu wa kawaida katika nafasi ya saba kwa alama 43. Washiriki wapya kabisa Menengai Oilers walijihakikishia msimu mwingine kwa kumaliza katika nafasi ya nane kwa alama 36.

Homeboyz, ambayo ilifika nusu-fainali katika makala mawili yaliyopita, iliridhika katika nafasi ya tisa mwaka huu kwa alama 29. Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ilifunga msimu katika nafasi ya 10 kwa alama 23.

Strathmore Leos na Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi ziliaga ligi hii ya klabu 12 kwa kumaliza katika nafasi mbili za mwisho baada ya kuzoa alama 14 na 11 mtawalia.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya Cup, timu zitapokea zawadi ya kifedha. Nambari moja hadi nne watatia kibindoni Sh1 milioni, Sh600,000, Sh400,000 na Sh300,000, mtawalia.