Michezo

Kabras RFC wasuka njama ya kuzima ukiritimba wa KCB kwenye raga ya Kenya Cup kuanzia 2020-21

October 24th, 2020 2 min read

CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI mpya wa timu ya Kabras Sugar RFC, Nzingaye Nyathi, analenga kusuka kikosi thabiti kitakachohimili ushindani mkali na kutwaa mataji mbalimbali ya raga humu nchini.

Hii ni baada ya mabingwa hao wa Enterprise Cup kujinasia huduma za wanaraga wawili wa haiba kutoka Afrika Kusini kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21. Wawili hao ni Ntokozo Vidima na Aphiwe Stemaz.

Vidima ana uwezo wa kuchezeshwa katika safu ya kati au pembezoni mwa uwanja na amewahi pia kuvalia jezi za Sharks, Free State Cheetahs na Border Bulldogs nchini Afrika Kusini. Kwa upande wake, Stemaz ni fowadi mahiri ambaye pia amewahi kuchezea Free State Cheetahs na Border Bulldogs.

Kwa mujibu wa Philip Jalango ambaye ni Mwenyekiti wa Kabras RFC, ujio wa wanaraga hao utainua viwango vya ushindani kambini mwa kikosi chake ambacho kimejiwekea malengo ya kutwaa mataji yote ya raga msimu ujao.

“Ni wachezaji wa haiba kubwa ambao wanaleta nguvu mpya na tajriba pevu itakayowapa wachezaji wetu uzoefu wa kutosha katika vipute mbalimbali,” akasema kwa kusisitiza kwamba klabu itakweza ngazi chipukizi watatu zaidi kuunga kikosi cha kwanza msimu ujao.

Vidima na Stemaz wanaendeleza orodha ndefu ya wanaraga raia wa Afrika Kusini kuwahi kuchezea Kabras ambao miaka miwili iliyopita, walijivunia huduma za Logan Basson, Claude Johannes na Mario Wilson.

Hadi kusitishwa kwa raga ya humu nchini mnamo Machi kutokana na janga la corona, Kabras walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 74 chini ya ukufunzi wa Henley Plessis wa Afrika Kusini. Walitarajiwa kuvaana na mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba RFC katika hatua ya nusu-fainali.

Kocha mpya wa Kabras RFC, Mzingaye Nyathi na msaidizi wake Felix Reyon walitua humu nchini mwishoni mwa mwezi huu kutoka Zimbabwe na Afrika Kusini mtawalia.

Wawili hao waliteuliwa kudhibiti mikoba ya Kabras kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja na wanatazamiwa kusuka njama ya kutamalaki kampeni za msimu ujao katika kivumbi cha Kenya Cup na mapambano mengine ya raga ya humu nchini.

Mwanaraga wa zamani wa Kenya Simbas, Edwin Achayo atadhibiti sasa mikoba ya chipukizi wa Kabras akisaidiana na Richard Ochieng ambaye pia ni kocha wa viungo. Jerome Paarwater ambaye ni kocha wa zamani wa Simbas ndiye Mkurugenzi wa Raga kambini mwa Kabras.

“Idadi kubwa ya wanaraga tuliowategemea msimu uliopita wamesalia kikosini na kiu ya kutamalaki vipute mbalimbali ingalipo. Tunatarajia kujivunia matokeo ya kuridhisha hata zaidi kuliko muhula uliopita,” akaongeza Jalango.

Miongoni mwa wanaraga mahiri watakaoendelea kutegemewa na wanasukari wa Kabras ni George Nyambua, Dan Sikuta, Asman Mugerwa, Hillary Odhiambo, Max Adaka, Brian Tanga, Felix Ayange na Nick Barasa.

Nyathi amesema kubwa zaidi katika maazimio yake ni kurejesha ubabe uliowawezesha Kabras kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya Cup mnamo 2016 na ufalme wa Enterprise Cup mnamo 2019.

Kabras wamezidiwa maarifa na wanabenki wa KCB katika fainali tatu zilizopita za Kenya Cup, rekodi mbovu ambayo Nyathi atapania kutamatisha.

“Bado sijafahamu uwezo wa kila mchezaji uwanjani kwa sababu hatufanyi mazoezi kutokana na janga la corona. Lakini napania kuwapa wachezaji wote nafasi sawa ya kudhirisha utajiri wa vipaji vyao katika idara mbalimbali uwanjani,” akasema.