Michezo

Kabras Sugar, KCB wataja silaha za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu katika fainali Kakamega

May 17th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Kabras Sugar na mabingwa watetezi KCB wametaja vikosi vyao vitakavyomenyana katika fainali ya Ligi Kuu ya Raga ya Kenya (Kenya Cup) ya msimu 2018-2019 uwanjani Kakamega Showground almaarufu ‘The Forest’ hapo Mei 18, 2019.

Kabras, ambayo inafukuzia taji lake la pili baada ya kuibuka bingwa katika msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu mwaka 2016, itatumia mwiba Philip Wokorach kutafuta muujiza wa kushinda wanabenki kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Vijana wa Henley Du Plessis, ambao walipata tiketi ya kuandaa fainali baada ya kumaliza msimu wa kawaida juu ya jedwali ya ligi hii ya klabu 12, wamepoteza mechi tisa na kutoka sare moja dhidi ya KCB ligini tangu waingie Ligi Kuu msimu 2014-2015.

Kabras kutoka kaunti ya Kakamega inashiriki fainali yake ya tano mfululizo, ingawa tatu kati ya fainali hizo ilipoteza dhidi ya KCB mwaka 2015, 2017 na 2018.

Ilipata taji lake la mwaka 2016 kwa kulemea Impala Saracens 22-5.

KCB ya kocha Curtis Olago inajivunia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2005, 2006, 2007, 2015, 2017 na 2018.

Wanabenki hawa, ambao walichabanga Kabras 44-20 katika msimu wa kawaida, walikabwa 15-15 ma wanasukari hawa walipozuru Kakamega mara ya mwisho mnamo Desemba 3, 2016.

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 49 fainali ya Kenya Cup inafanyika nje ya Nairobi.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande – Daniel Sikuta (Kabras Sugar) na Andrew Amonde, Jacob Ojee na Vincent Onyala kutoka KCB watashiriki mchuano huu kabla ya kuelekea barani Ulaya kwa duru mbili za mwisho za Raga ya Dunia zitakazofanyika nchini Uingereza hapo Mei 25-26 na Ufaransa mnamo  Juni 1-2, mtawalia.

Vikosi:

KABRAS SUGAR

1. Ephraim Oduor, 2.Maxwell Adaka, 3.Asuman Mugerwa (Uganda), 4.Charlton Mokua, 5. Hillary Odhiambo 6.Daniel Sikuta, 7.George Nyambua, 8. Claude Johannes (Afrika Kusini), 9. Barry Robinson, 10.Philip Wokorach (Uganda), 11. Kevin Keegan, 12. Nick Baraza, 13. Mario Wilson (Afrika Kusini) 14.Felix Ayange 15. Jone Kubu (Fiji). Wachezaji wa akiba – 16. Geoffrey Shitambasi, 17. Hillary Mwanjilwa, 18. Joseph Odero, 19. Brian Juma, 20. Kevin Kabole, 21. Dan Angwech, 22. Johnstone Mung’au, 23. Paul Abuto. Wachezaji wa ziada – 1. Bramwell Mayaka, 2. Eugene Sifuna.

KCB 

1. Oscar Simiyu Sorano, 2.Peter Karia, 3.Curtis Lilako (nahodha), 4.Oliver Mang’eni, 5.Francis Mwita, 6.Andrew Amonde, 7.Peter Waitere, 8.Davis Chenge, 9.Samuel Asati, 10.Ken Moseti, 11.Jacob Ojee, 12.Brian Omondi, 13.Peter Kilonzo, 14. Tony Onyango, 15.Isaac Njoroge. Wachezaji wa akiba – 16.Griffin Musila, 17.Moses Amusala, 18.George Gichure, 19.Brian Nyikuli, 20.Rocky Aguko, 21.Michael Wanjala, 22.Shaban Ahmed, 23.Vincent Onyala.