Michezo

Kabras Sugar nje, MMUST ndani Kakamega Sevens ikianza

July 21st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI wa duru ya ufunguzi ya mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya kitaifa ya Kakamega Sevens, Kabras Sugar na Western Bulls, walishindwa kuingia robo-fainali Jumamosi mjini Kakamega.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) wameshangaza katika siku ya kwanza ya duru hii baada ya kubwaga mabingwa wa Kenya mwaka 2017 Kabras 24-5 na Kisii 29-0 na kujikatia tiketi ya robo-fainali kutoka Kundi C.

MMUST, ambao walianza kampeni kwa mguu mbaya walipokung’utwa 36-10 na mabingwa wa Ligi Kuu KCB kabla ya kujinyanyua, wanaungana na Mwamba, KCB, Homeboyz, Impala Saracens, Nondies, Nakuru na Strathmore Leos robo-fainali zitakazosakatwa Jumapili.

Timu kubwa ambazo zimeshindwa kuingia mechi za mduara wa nane-bora ni Kenya Harlequin, ambao wamepoteza mechi zao zote za Kundi D dhidi ya malimbukeni Strathmore Leos 24-14, Egerton Wasps 10-0 na mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 2013 na 2014 Nakuru 19-7, na wafalme wa Ligi Kuu mwaka 2016 Kabras.

St Peter’s Mumias ilinyakua ubingwa wa kitengo cha Shule za Upili baada ya kulipua Kakamega 26-7.

Ni mara ya kwanza kaunti ya Kakamega ni mwenyeji wa duru ya mashindano haya ya kitaifa yaliyoanzishwa mwaka 1999. Kuondolewa kwa Kabras na Bulls, ambayo itarejea kwenye Ligi Kuu msimu ujao wa 2019-2020 baada ya kupandishwa daraja, hata hivyo hakujaacha Kakamega bila mwakilishi. MMUST inapatikana katikati mwa mji wa Kakamega.  

Matokeo ya siku ya kwanza:

Kundi A

Impala Saracens 17-10 Menengai Oilers

Homeboyz 27-5 Western Bulls

Impala Saracens 26-5 Western Bulls

Homeboyz 17-7 Menengai Oilers

Menengai Oilers 20-7 Western Bulls

Homeboyz 12-12 Impala Saracens

 

Kundi B

Nondies 7-5 Mean Machine

Mwamba 38-0 Kisumu

Nondies 24-10 Kisumu

Mwamba 19-0 Mean Machine

Mean Machine 24-5 Kisumu

Mwamba 26-12 Nondies

 

Kundi C

Kisii 5-21 Kabras Sugar

KCB 36-10 MMUST

Kabras Sugar 5-24 MMUST

KCB 42-0 Kisii

Kisii 0-29 MMUST

KCB 29-7 Kabras Sugar

 

Kundi D

Kenya Harlequin 14-24 Strathmore Leos

Nakuru 41-7 Egerton Wasps

Kenya Harlequin 0-10 Egerton Wasps

Nakuru 15-0 Strathmore Leos

Strathmore Leos 26-0 Egerton Wasps

Nakuru 19-7 Kenya Harlequin