Michezo

Kabras Sugar wasalia mbele Kenya Cup kwa alama 15 zaidi

November 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAFALME wa mwaka 2016 Kabras Sugar na mabingwa watetezi KCB wako bega kwa bega juu ya Ligi Kuu ya raga (Kenya Cup) ya msimu 2019-2020 kwa alama 15, baada ya kuandikisha ushindi wa tatu mfululizo wikendi.

Wanasukari wa Kabras wanashikilia nafasi ya kwanza kwa ubora wa alama baada ya kulipua mabingwa wa zamani Impala Saracens kwa alama 27-3 uwanjani Kakamega Showground.

Wanabenki wa KCB, ambao wanafukuzia taji la nne mfululizo, walilima washindi wa mwaka 2013 na 2014 Nakuru 50-13, uwanjani Ruaraka na kurukia nafasi ya pili kutoka nambari tatu.

KCB ilinufaika kupiga hatua moja mbele pale Impala iliyoshikilia nafasi ya pili ilipoteleza dhidi ya Kabras na kupoteza alama muhimu.

Vilevile, Homeboyz ilifaidika na masaibu ya Impala ikiimarika kutoka nafasi ya tano hadi nambari tatu baada ya kulipua Menengai Oilers 25-20 uwanjani Jamhuri. Homeboyz, ambayo pamoja na Kabras na KCB ndizo klabu hazijapoteza mchuano msimu huu, imezoa alama 13.

Oilers ilipata alama moja ya bonasi kwa kupoteza pembemba dhidi ya Homeboyz. Alama hiyo ilihakikisha Oilers inakwamilia nafasi ya nne kwa jumla ya alama 11.

Impala ilitupwa chini nafasi tatu hadi nambari tano. Imezoa alama 10, sawa na nambari sita Mwamba iliyolipua Kisumu 65-22, uwanjani Impala Grounds. Impala iko mbele ya Mwamba kwa tofauti ya ubora wa alama.

Mabingwa mara 17 Nondies wameruka juu nafasi moja hadi nambari saba baada ya kuzoa ushindi wao wa kwanza msimu huu kwa kulaza wenyeji Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta 38-25.

Nondies wana alama sita, alama moja zaidi ya nambari nane Western Bulls kutoka kaunti ya Kakamega walioshangaza washindi mara nane Kenya Harlequin 21-19 baada ya kutoka chini 0-19 wakati wa mapumziko uwanjani RFUEA jijini Nairobi.

Ushindi wa Bulls uliopatikana kupitia kwa miguso na mikwaju ya miguso hiyo kutoka kwa Derrick Ashiundu, uliiwezesha kupaa nafasi mbili.

Kuimarika kwa Nondies na Bulls kulisababishia Kisumu madhara ya kuteremka nafasi mbili hadi nambari tisa. Kisumu imezoa alama nne. Inafuatiwa na Blak Blad, Harlequin na Nakuru katika nafasi tatu za mwisho, mtawalia.

Blak Blad, Harlequin na Nakuru hazijashinda mechi msimu huu. Blak Blad imezoa alama mbili nazo Harlequin na Nakuru zimeambulia alama moja. Kwingineko, timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa ilirejea nchini Jumapili jioni kutoka Afrika Kusini ilikoshinda Kombe la Afrika na kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka 2020.

Ratiba ya mechi zijazo za Kenya Cup (Novemba 16): Nakuru na Kenya Harlequin, Menengai Oilers na KCB, Homeboyz na Western Bulls, Impala Saracens na Mwamba, Nondies na Kabras Sugar, Blak Blad na Kisumu.