Michezo

Kabras Sugar yafanikiwa kuibwaga KCB katika raga wachezaji 15 kila upande

December 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KABRAS Sugar hatimaye imeonja ushindi wake wa kwanza dhidi ya KCB kwenye raga ya wachezaji 15 kila upande baada ya kuchabanga wanabenki hao ugenini 19-6 uwanjani Ruaraka jijini Nairobi, Jumamosi.

Wanasukari wa Kabras, ambao walikuwa wamechapwa mechi tisa na kutoka sare mara moja dhidi ya KCB tangu waingie Ligi Kuu (Kenya Cup) mwaka 2014, waliongoza 7-0 kupitia mguso wa Mganda Asuman Mugerwa ulioandamana na mkwaju wa Mfiji Jone Kubu. KCB ilipunguza mwanya huo hadi 7-3 kupitia penalti ya Levi Amunga.

Hata hivyo, Mfiji Timoci Sinaite aliimarisha uongozi wa Kabras hadi 12-3 baada ya kupachika mguso, huku Kubu akikosa mkwaju.

Amunga aliongeza penalti nyingine baada tu ya Kabras kusalia wachezaji 14 uwanjani wakati Hillary Odhiambo alilishwa kadi ya njano kabla ya Mugerwa kuhitimisha na mguso uliohakikisha Kabras inalipiza kisasi ambacho imekuwa ikitafuta kwa muda mrefu.

Matokeo haya yanamaanisha kuwa Kabras sasa ndio klabu pekee haijapoteza mechi kwenye ligi hii ya timu 12 msimu huu. Mabingwa watetezi KCB waliingia mchuano huu wakiwa timu nyingine ambayo haikuwa imepoteza mechi.

Katika matokeo ya mechi zingine zilizosakatwa Jumamosi, Kenya Harlequin ililemewa 15-13 na Mwamba mbele ya mashabiki wake uwanjani RFUEA, Nakuru ikaliza wageni wake Impala Saracens 30-20 uwanjani Nakuru Athletic, nayo Menengai Oilers ikatumia uwanja wake wa nyumbani wa Nakuru Showground kulima Nondies 27-3. Homeboyz ilipepeta Blak Blad ya Chuo Kikuuu cha Kenyatta 32-22 uwanjani Jamhuri nayo Western Bulls ikazima Kisumu 23-5 mjini Kakamega.

Takwimu za ana kwa ana kati ya KCB na Kabras Sugar:

Novemba 8, 2014 – KCB 13 Kabras Sugar 3 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Machi 14, 2015 – KCB 27 Kabras Sugar 3 (fainali ya ligi, RFUEA)

Desemba 19, 2015 – KCB 40 Kabras Sugar 15 (msimu wa kawaida wa ligi, Railway Club Nairobi)

Juni 18, 2016 – KCB 24-12 Kabras Sugar (fainali ya Enterprise Cup)

Desemba 3, 2016 – Kabras Sugar 15 KCB 15 (msimu wa kawaida wa ligi, Kakamega)

Januari 28, 2017 – KCB 22 Kabras Sugar 17 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Aprili 22, 2017 – KCB 36 Kabras Sugar 8 (fainali ya ligi, Ruaraka)

Februari 24, 2018 – KCB 41 Kabras Sugar 12 (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)

Machi 24, 2018 – KCB 29 Kabras Sugar 24 (fainali ya ligi, Ruaraka)

Februari 23, 2019 – KCB 44 Kabras Sugar 20 (msimu wa kawaida wa ligi, Impala)

Mei 18, 2019 – Kabras Sugar 15 KCB 23 (fainali ya ligi, Kakamega)

Novemba 30, 2019 – KCB 6-19 Kabras Sugar (msimu wa kawaida wa ligi, Ruaraka)