Michezo

Kabras Sugar yatumia uwanja wa nyumbani vyema kwa kuipiga Mwamba 56-13

February 1st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU za Kabras Sugar, KCB, Homeboyz, Blak Blad na Menengai Oilers zilitumia viwanja vyao vyema kwenye Ligi Kuu ya Raga nchini (Kenya Cup) Jumamosi.

Uwanjani Bull Ring mjini Kakamega, Kabras iliongeza Mwamba katika orodha ya klabu imepiga msimu huu wa 2019-2020 baada ya kuchapa timu hiyo kutoka Nairobi 56-13.

Viongozi hao wa ligi hii ya klabu 12 walienda mapumzikoni wakiwa mbele 33-3. Kwa jumla, wenyeji Kabras walipata miguso minane ambayo yote iliandamana na mikwaju yake, huku Deus Mudaki akifunga mguso wa pekee wa Mwamba zikisalia dakika 10 mechi itamatike.

Timu ya Homeboyz ililipua Nakuru almaarufu Wanyore 47-5. Homeboyz ilienda mapumzikoni kifua mbele 28-0 baada ya kupata miguso minne ikiwemo kutoka kwa Leonard Mugaisi, Michael Wanjala na Joshua Chisanga pamoja na mikwaju kutoka kwa Evin Asena.

“Madeejay” hao waliendelea kutesa Nakuru katika kipindi cha pili wakipata miguso miwili dhidi ya mguso wa kujifariji kutoka kwa Philip Kwame.

Mechi kati ya Nondescripts na Kisumu, ambayo pia iliratibiwa kuchezewa Jamhuri Park, iliahirishwa Ijumaa baada ya timu ya Kisumu kuhusika katika ajali ya barabarani ikielekea Nairobi kumenyana na mabingwa hao wa mataji 17.

Katika matokeo mengine ya Februari 1 mabingwa watetezi KCB walipepeta Kenya Harlequin 29-3 uwanjani Ruaraka nao Menengai Oilers wakabwaga Western Bulls 43-17.