Habari Mseto

SACHANGWAN: Kaburi la umma lilivyogeuka kitega uchumi kwa wenyeji

January 31st, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

JAPO ukiwa na upande wake mbaya wa kuwapokonya watu wapendwa wao na kuziacha familia na vidonda visivyopona rohoni, mkasa wa moto wa Sachangwan uliotokea mnamo 2009 ulifungua ukurasa mwingine kwa wakazi wa eneo hilo.

Ulipotokea mkasa huo, eneo hilo lilikuwa msitu ambapo ilikuwa vigumu kuwapata watu.

Hata hivyo, baada ya watu 78 waliokufa kwenye mkasa kuzikwa katika kaburi la pamoja, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Eldoret, eneo hilo sasa limegeuka soko ambalo ni kitega uchumi kwa vijana na kina mama.

Kando tu ya kaburi ambapo mabaki ya watu 78 walilazwa, makumi ya vijana na kina mama huamka kila siku kwenda kuuza miwa, vinywaji na vyakula kwa wasafiri na watu wanaosimama kaburini kujitazamia matokeo ya mkasa huo.

Unapofika tu katika kaburi hilo, utawapata vijana waliobeba miwa iliyotayarishwa huku wakiuzia wasafiri kwenye magari, nao kina mama kando ya barabara aidha wakiandaa chakula ama kuwahudumia wateja wao.

“Huwa nauza chapati, Githeri, wali na chai. Kwa kawaida naanza kujiandaa asubuhi na kufikia saa tano niko hapa naanza kuwauzia wateja. Napata kitu kidogo cha kuwahudumia watoto kutokana na biashara hii kwani nina wajukuu ambao wanasoma,” Bi Esther Kirui, mama wa miaka 58 akaeleza Taifa Leo.

Bi Kirui alianza biashara hiyo eneo hilo, ambalo linafahamika kama ‘Kaburini’ kwa wakazi mnamo 2013, japo alikuwa akiuzia katika barabara hiyo, katika eneo tofauti.

“Hapa ninauzia watu mbali mbali, hawa wanaouza miwa, wasafiri wa mabasi na malori. Pia ninawauzia maziwa aina ya Mursik na wanapenda sana,” akasema.

“Kabla ya mkasa na kaburi hili kujengwa, hizi biashara hazikuwapo hapa. Ni kaburi ambalo liliwavuta watu kuuzia hapa kwani watu wanasimama hapa kwa wingi,” Bi Kirui akasema.

Bi Jackline Jepkoech pia amekuwa eneo hilo la ‘Kaburini’ akifanya biashara ya kuza miwa kwa miaka mitatu sasa.

“Nauza miwa hapa Kaburini na biashara hii imetusaidia sana kwani tunapata chakula na kuweza kuwasomesha watoto na tunapata vitu vingi,” Bi Jepkoech mwenye umri wa miaka 30 anasema.

“Huwa malori yanatuletea hadi hapa na kutuuzia kisha nasi tunaandaa na kuuzia wasafiri ama watu wanaokuja kutazama kaburi hapa. Si biashara mbaya kwani imekuwa ikitushikilia,” akasema.

Hata hivyo, ndani yake anafahamu kuwa babake ni mmoja wa watu waliokufa katika mkasa huo wa moto, naye kakake pia aligongwa na gari akiuza miwa hapo na kufariki mwaka uliopita.

Sehemu hiyo ina zaidi ya wauzaji 20 wa vitu tofauti na ambao wameshikamana ili kujiinua kwa kuunda chama ambapo wanatoa pesa kila siku na kumpokeza mmoja wao, japo pia kunazo changamoto ambazo wanakumbana nazo.

“Kama tungejengewa mahali ambapo pana kivuli, tungesaidika sana kwani hapa ni mahali wazi ambapo jua likiwa tunachomwa sana. Aidha, mvua inaponyesha huwa ni shida, tunaenda pale kwa kaburi kujikinga hata kula tunakulia huko,” akasema Bi Kirui.

Lakini hata eneo hilo la kaburi bado lina changamoto zake kwani hakuna choo ambapo watu wanaweza kujisaidia, licha ya idadi kubwa ya watu ambao mara kwa mara hushuka pale kujionea, na pia wafanyabiashara hao ambao hushinda pale kutwa nzima.

“Wakati kaburi lilijengwa, kandarasi ilikuwa pia kujengwe vyoo, eneo hili liwe na maji na kuwe na bawabu wa kulichunga. Hata hivyo, bawabu aliyeajiriwa hakulipwa hadi akaacha kazi, kwa sasa hata lango la kaburi liliibiwa,” akasema Bi Rachael Maru, MCA Maalum kutoka eneo hilo.

Bi Maru alisema kuwa japo watu hutoka maeneo mbalimbali kujitazamia kaburi hilo, huwa wanalazimika kwenda haja msituni, akisema “vyoo vingekuwepo vingewasaidia vijana na kina mama kupata pesa kidogo za kujisaidia.”