Kadha wanusurika kifo baada ya basi kupoteza mwelekeo Thika Road

Kadha wanusurika kifo baada ya basi kupoteza mwelekeo Thika Road

Na SAMMY WAWERU

ABIRIA kadha walinusurika kifo kwa tundu la sindano Alhamisi jioni baada ya basi walimokuwa kupoteza mwelekeo na kuingia kwenye mtaro wa majitaka katika barabara kuu ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Carwash, kati ya mtaa wa Githurai na Roysambu, ilihusisha basi la kampuni ya uchukuzi ya Virginia.

Kulingana na walioshuhudia, abiria kadha walipata majeraha.

“Huenda breki zilikuwa na tatizo likapoteza mwelekeo, dereva akijaribu kukwepa kugonga gari lililokuwa mbele yake akaingia kwenye mtaro wa majitaka,” akasema mmoja wa walioshuhudia.

La kushangaza basi hilo lilikuwa katika leni ya kuchukua na kushusha abiria (service lane).

“Inavyoonekana alikuwa kwa mwendo wa kasi,” akasema dereva wa matatu moja inayohudumu kati ya Roysambu na mtaa wa Ruiru.

Ilichukua zaidi ya muda wa saa moja kuondoa basi hilo lililokwama kwenye mtaro wa majitaka, ulio kati ya service lane na ile ya kasi, na ambalo wahudumu wake walificha nambari za usajili kwa kufunika kwa mavazi.

Maafisa wa trafiki waliofika eneo la mkasa walihimiza madereva kupunguza kasi ya magari na matatu wakiwa katika leni ya kuchukua na kushusha abiria.

Ni leni ambayo mara nyingi hutumiwa na wahudumu wa bodaboda, wengine wakienda kinyume na mwelekeo wa magari.

You can share this post!

Chelsea yaibuka Klabu Bora ya Mwongo kati ya 2011 na 2020

Safari ya David Makui kuwa milionea baada ya elimu yake...