Habari Mseto

Kadhaa wanusurika kifo katika ajali Thika Superhighway

November 5th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WATU kadhaa walinusurika kifo katika ajali iliyotokea Jumatatu jioni katika barabara ya Thika Superhighway.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Githurai, ilihusisha magari manne: basi, gari aina ya probox, pickup na gari lingine la mmiliki binafsi.

Kulingana na walioshuhudia, basi linalohudumu baina ya mtaa wa Githurai na jiji la Nairobi, lilinuwia kuingia barabara ya kasi ambapo lilikutana na probox ambayo pia ilikuwa ikiingia.

“Probox iligongwa na kusukumwa upande wa barabara ya kasi, ikashirikisha magari mengine mawili,” akasema mmoja wa walioshuhudia.

Gari hilo aina ya probox lilikuwa na watu watatu. Mwanamke mmoja alipata majeraha na kupelekwa katika kituo kimoja cha afya kilichoko karibu.

Afisa mmoja wa trafiki na aliyeomba jina lake lisichapishwe kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na wanahabari, amewataka maderava kuwa waangalifu wanapoingia barabara ya mwendo wa kasi

“Thika Superhighway ina njia nne, mbili za kuelekea jijini Nairobi na zinazoelekea Thika. Sheria za barabara ni wazi dereva anapotaka kuingia ile ya kasi, katika viingilio rasmi, akague kwa makini mkono wake (akimaanisha wa kulia),” akashauri.

Alisema ubadilishaji holela wa leni pia ni hatari.

Barabara hiyo si geni katika visa vya ajali, hasa iingiapo Ijumaa jioni na mnamo wikendi. Ajali nyingi zinahusishwa na uendeshaji wa magari kwa mwendo wa kasi, licha ya ilani nyingi zilizowekwa.

Unywaji wa pombe na utumiaji wa simu miongoni mwa madereva pia unalaumiwa.

Mabasi yanayohudumu kati ya Githurai na jiji la Nairobi yanatajwa kuwa tepetevu, na mwaka 2019 visa kadhaa vya ajali zinazohusishwa nayo vimeripotiwa.

Agosti 2019 basi moja linalomilikiwa na kampuni ya Zam Zam, nambari za usajili KCC 021A, kondakta wake alidaiwa kurusha nje mwanamume, Gerald Kamotho eneo la Roysambu gari likiwa kwa mwendo wa kasi.

Mshukiwa alitoroka na licha ya dereva kukamatwa, aliachiliwa kwa dhamana ya polisi pamoja na basi hilo.

Gari lilo hilo mwaka 2018 pia lilidaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi wa Taasisi ya NIBS, bewa la Ruiru.