Michezo

Kadi kuwakosesha mastaa 3 mechi za KPL

July 10th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

HUKU wiki ya 23 ya ligi kuu nchini KPL ikitarajiwa kunogeshwa wikendi hii ya Tarehe 14 na 15, wanadimba watatu wanaotegemewa na klabu zao watakosa kuziwajibikia kutokana na swala la nidhamu katika mechi za awali.

Kiungo wa AFC Leopards Whyvonne Isuza ambaye amekuwa na msimu wa kuridhisha  atakosa nafasi ya kuwajibikia Ingwe Jumamosi,14  watakapochuana dhidi ya Bandari FC baada ya kupata kadi tano za manjano  kwenye mechi waliyoishinda 1-0 ya Jumapili, 8 dhidi ya SoNy Sugar.

Bao la ushindi kwenye mtanange huo ulitiwa wavuni na mlinzi matata wa Ingwe Abdalla Salim.

Vihiga United pia watakosa mchezaji wao muhumu Christopher Masinza ambaye pia idadi ya kadi za manjano alizolishwa zimefikia tano.

Masinza alifunga bao muhimu lililowapa ushindi Vihiga United walipochuana na limbukeni  Wazito FC katika mechi ya siku ya Jumapili, 8.

Atakosa mechi itakayowakutanisha na  Ulinzi Stars katika uwanja wa Mumias Complex kwenye Kaunti ya Kakamega Jumapili, 15.

Mlinzi wa Sofapaka raia wa Burundi Moussa Omar pia hajasazwa na marufuku iyo hiyo ya kupokezwa kadi tano ya manjano ya hivi punde ikiwa ni katika ushindi wao  Jumapili, 8 dhidi ya Mathare United.

Ellie Asiche, Kepha Aswani na Piston Mutamba ndiye walikuwa wafungaji katika mechi hiyo iliyosakatwa  uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.