Michezo

Kadi nyekundu zatema wachezaji 4 nje ya KPL

August 8th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

WACHEZAJI wanne wanatarajiwa kukosa mechi za ligi ya KPL Jumamosi na Jumapili baada ya kulishwa kadi nyekundu moja kwa moja au kupokezwa kadi mbili ya manjano kisha kadi nyekundu.

Kiungo wa Bandari Fred Nkata atajiunga na kiungo wa Tusker Boniface Muchiri na mwenzake wa AFC Leopards Whyvone Isuza katika orodha ya wachezaji watakaokosa mechi hizo.

Mshambulizi wa Zoo Kericho FC Earnest Kipkoech pia atakosa mechi yao ya raundi ya 26 nyumbani dhidi ya Nzoia Sugar siku ya Jumapili.

Kipkoech atajiunga na mshambulizi mwenzake Nicholas Kipkurui anayetumikia marufuku ya mechi tatu baada ya kupokezwa kadi ya tano ya manjano.

Isuza wa AFC leopards alilishwa kadi mbili za manjano katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Mathare United na atakosa mechi dhidi ya Nakumatt FC na Thika United FC.

Nkata alitimuliwa katika ushindi wa 2-1uliosajiliwa na Bandari dhidi ya Mabingwa watetezi Gor Mahia siku ya Jumanne.

Atakosa mechi ya Jumapili ugeni dhidi ya Tusker ambao pia hawatakuwa na huduma za kiungo wao Boniface Muchiri.