Habari za Kitaifa

Kaende kaende: Vyama vya walimu vyaidhinisha mgomo na kuweka mitihani hatarini


MITIHANI ya Kitaifa itakayofanyika muhula wa tatu huenda ikavurugika baada ya walimu na wahadhiri kutishia kuandaa mgomo wakitaka nyongeza ya mshahara.

Shule na vyuo vikuu nchini vimeratibiwa kufungiliwa mwishoni mwa mwezi huu na mapema mwezi ujao mtawalia. Wanafunzi wanaofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Nchini (KCSE) wataanza mtihani wao Oktoba na huenda ndio wataathirika zaidi na mgomo huo iwapo utafanyika.

Masomo na muda wa kudurusu kwa watahiniwa hao utavurugwa iwapo walimu watakuwa wakishiriki mgomo. Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu Nchini (UASU) ndio wa hivi punde kutoa notisi ya kushiriki mgomo wakilalamikia kucheleweshewa mishahara yao.

Baadhi ya vyuo vikuu navyo havijalipa mishahara kwa wafanyakazi wao na masomo huenda yakavurugika vyuo vikuu vikifunguliwa mnamo Septemba.UASU ilitoa notisi hiyo mnamo Jumatano baada ya kuandaa mkutano wa baraza lake kuu.

Katibu Mkuu Dkt Constantine Wasonga amesema kuwa vyuo vikuu vimeendelea kuchelewesha mishahara ya wahadhiri na hata vikilipa, havilipi hela zote.

Dkt Wasonga alisema kuwa vyuo vikuu navyo pia havijakuwa vikiwasilisha makato ya mikopo, pensheni na makato mengine licha ya kuyaondoa kwenye mshahara wao.

Tishio la UASU la kuandaa mgomo linakuja wiki moja baada ya Chama cha Walimu Nchini (KNUT) na Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) kutangaza kuwa mgomo wa walimu nchini utaanza Agosti 26.

Hii ndiyo tarehe ambapo shule zitakuwa zikifunguliwa kwa muhula wa tatu. Kuppet mnamo Jumatatu iliwasilisha malalamishi yake kwa Waziri wa Leba, Dkt Alfred Mutua, ikisema kuwa haiwezi kuyasuluhisha kwa Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC).

Knut pia iliwasilisha malalamishi yake kwa Dkt Mutua mnamo Jumatano baada ya kuandaa mkutano na waziri huyo Jumanne.

Miungano ya walimu imekuwa ikitaka malipo ya awamu ya pili ya makubaliano ambayo walikuwa nayo na serikali maarufu kama CBA (2021-2025).

Makubaliano hayo yalisheheni matakwa yao ambapo walimu wakufunzi 46,000 waliokuwa wameajiriwa kupitia kandarasi, wangepewa ajira ya kudumu. Pia walimu 130,000 wangepandishwa vyeo.

Mgomo huo ni makaribisho mabaya kwa waziri mpya wa elimu Julius Ogamba. Ukifanyika basi maandalizi ya mtihani na kufanyika kwake kutavurugika zaidi.Vyuo vikuu navyo havijasazwa vikiendelea kuandamwa na madeni mengi ambayo sasa yamefikia Sh84 bilioni.

Mgao ambao walikuwa wakiupata kutoka kwa serikali nao ulipunguzwa baada ya serikali kukumbatia mfumo mpya wa ufadhili.

“Si jambo la haki kwa serikali kuendelea kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi kwenye vyuo vikuu vya umma kila mwezi. Hii imesababisha ukosefu wa heshima na aibu kwa wanachama wetu,” akasema Dkt Wasonga.

Alitaja Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK) aliyodai iliwalipa wahadhiri asilimia 65 ya mshahara wao mnamo Julai.

“TUK wamevuka mpaka na natoa wito kwa wanachama wetu chuoni humo waandae mgomo. Kuanzia Septemba hakutakuwa na masomo ya chuo kikuu nchini kwa sababu serikali inaona kama tunafanya mzaha,” akaongeza.

Dkt Wasonga aliwakashifu Manaibu Chansela kwa kutomwambia Rais William Ruto kuwa mfumo wa kutoa mgao kwa vyuo vikuu mwaka ujao haufanyi kazi na unalemeza vyuo kifedha.