Habari

Kaeni chonjo

March 14th, 2020 2 min read

MARY WANGARI na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameanza kuchukua hatua zaidi za tahadhari baada ya kisa cha kwanza cha virusi vya corona nchini kuthibitishwa na Serikali Ijumaa.

Kuanzia madukani, kwenye matatu na kazini, Wakenya walianza kuwa makini kujikinga wasiambukizwe virusi hivyo huku maafisa wa Wizara ya Afya wakifuatilia safari za mwathiriwa huyo tangu aliporejea nchini kutoka Amerika siku kumi na mbili zilizopita.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alifichua kwamba, mwathiriwa ni mwanamke, raia wa Kenya aliyerejea nchini Machi 5 kutoka Amerika kupitia Uingereza.

Mataifa hayo yameripoti maambukizi na vifo kutokana na corona.

“Wakenya wenzangu, ninataka kuwafahamisha kwamba Wizara ya Afya imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya corona,” alisema.

Ilibainika kuwa mwanamke huyo aliyekuwa akiishi eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado alitembelea jamaa zake eneo la Kitale.

Ijumaa, wasimamizi wa maduka ya Tuskys walisema walichukua hatua za tahadhari kuhakikisha usalama wa wateja wao huku Wakenya wakifurika katika maduka makubwa kununua bidhaa na vifaa vya kujikinga.

Taarifa ya maduka hayo ilishauri Wakenya kutokuwa na hofu ya uhaba wa bidhaa kwa sababu kuna hifadhi ya kutosha.

Miongoni mwa bidhaa ambazo Wakenya waliwania ni sabuni na karatasi shashi na vyakula wakihofia kutengwa kwa baadhi ya miji inapofanyika katika mataifa mengine.

Wahudumu wa matatu pia walianza kuchukua hatua kwa kununua sabuni ya kusafisha mikono na kuhakikisha abiria wanaitumia kabla ya kupanda magari yao.

Waziri Kagwe alieleza kuwa mgonjwa huyo alikuwa amepata nafuu lakini hangeruhusiwa kuondoka katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) anakotibiwa, hadi atakapothibitishwa kutokuwa na virusi hivyo.

“Kiwango cha joto mwilini mwake kimeshuka hadi kufikia kiwango cha kawaida. Amerejelea hali ya kawaida, anakula lakini hawezi kuruhusiwa kuondoka hadi atakapopimwa na kupatikana hana virusi hivyo,” alifafanua.

Waziri huyo alisema serikali imeanza juhudi za kuwasaka watu wote waliotangamana na mgonjwa huyo alipoingia nchini.

Bw Kagwe alipuuzilia mbali dhana kuwa Waafrika hawaambukizwi virusi vya corona kutokana na rangi yao nyeusi akithibitisha kwamba mgonjwa huyo ni Mwafrika mwenye umri wa miaka 27.

Tangazo hilo liliashiria mwanzo wa nyakati ngumu kwa Wakenya huku serikali ikionekana kuanzisha juhudi za kuzuia mkurupuko huo kusambaa zaidi nchini.

Ijumaa, serikali ilitangaza kuwa maafisa wa usalama watasaidia Wizara ya Afya kukabiliana na virusi hivyo.

Serikali iliamrisha sehemu zote za ibada kuwapa waumini wao vifaa vya kunawa mikono. Ziara za kuwatembelea wafungwa gerezani pia zilisitishwa kwa muda wa mwezi mmoja ujao huku safari katika mataifa ya kigeni zikisitishwa ila tu zilizo muhimu huku safari katika mataifa yaliyoathiriwa zaidi zikipigwa marufuku.

Wakenya wametahadharishwa dhidi ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii au kueneza habari za kupotosha zinazoweza kuibua hofu na taharuki.

Ili kuhakikisha Wakenya watakuwa chonjo kila wakati, Wizara ya Afya ilisema kwamba itakuwa ikituma jumbe kila siku kuhusu mkurupuko huo.

Aliwahakikishia Wakenya kwamba, hakuna sababu ya kuwa na hofu na kuwahimiza kuendelea na maisha yao kama kawaida.

“Kwa sasa, tulicho nacho ni kisa cha vipimo vilivyothibitisha virusi vya corona. Si zaidi ya hiyo. Hivyo basi Wakenya wataishi kama kawaida, unapokwenda nenda kama kawaida, endelea na shughuli zako kama kawaida, nenda madukani kama kawaida, hakuna sababu ya kuwa na hofu,” alisema.

Huku akionekana kudokeza kuhusu nyakati ngumu zinazowasubiri Wakenya, Waziri alihimiza kila mwananchi kuwajibika binafsi huku akitoa wito kwa wafanyabiashara na mashirika ya kibinafsi kushirikiana na Wakenya katika kipindi hiki na kujiepusha na kujinufaisha kutokana na janga hili.

“Huu ni ule wakati tunapohimiza kuwajibika kwa dhati kutoka kwa raia. Hii si ile hali watu hutazama tu serikali, ni hali ambapo raia huwajibika. Wafanyabiashara na sekta za kibinafsi wanahimizwa kuchukua nafasi yao kwa kushirikiana na Wakenya katika maeneo yote.”

Baadhi ya Wakenya waliilaumu serikali kwa kutojitahidi vya kutosha kuzuia virusi hivyo, hasa kwa kuruhusu abiria kutoka mataifa yaliyoathiriwa na mkurupuko huo kuingia nchini kabla ya kutengwa kwa siku 14.