Habari Mseto

KAFYU: Dereva aua polisi akihepa kunaswa na polisi mwingine

April 15th, 2020 1 min read

Na John Njoroge

AFISA wa polisi alifariki Jumapili jioni akiwa kazini baada ya kugongwa na gari dogo lililokuwa likiendeshwa kwa kasi katika kizuizi cha Salgaa kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Afisa huyo alikuwa kazini katika kizuizi hicho wakati dereva huyo alipokuwa akiharakisha ili kuepukana na saa za marufuku ya kafyu asinyakwe na polisi. Aligongwa muda mfupi kabla YA saa moja jioni.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru Stephen Matu, akidhibitisha tukio hilo alisema afisa huyo alikuwa kazini akifuatilia wale ambao hawakuzingatia saa za kafyu alipogongwa na kufariki papo hapo.

Afisa huyo alithibitishwa kufariki alipofikishwa hospitali ya PNN, Nakuru.

Matu alisema dereva huyo alisimama baada ya ajali na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Salgaa ambapo aliandikisha taarifa na kuachiliwa kwa dhamana.