Habari Mseto

KAFYU: Hali halisi ya maisha mitaani

April 2nd, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Justus Masika anakadiria hasara kubwa katika biashara yake ya kuandaa na kuuza vyakula katika kibanda kimoja mtaani Kariobangi South Civil Servants jijini Nairobi tangu kafyu ya kuzuia uenezaji wa virusi vya corona ianze Machi 27.

Masika alijaribu bahati yake katika kazi ya uashi (mjengo), kuchuuza kahawa, kuuza matunda, kuuza miwa, kuuza maji na kuuza nguo za mitumba bila mafanikio nyakati tofauti kabla ya kuanzisha biashara ya hoteli mwaka 2018 baada ya kupata kibanda mtaani hapa kukopa pakiti mbili za unga wa ngano.

Anasema hali imekuwa ngumu tangu kafyu ianze kwa sababu wateja wamepunguka. Hii imemlazimu apike chapati kati ya 120 na 130 kila siku. Kabla ya kafyu kuanza, alikuwa akipika chapati 360 kila siku. “Nilikuwa napika bandali nzima (pakiti 12) kila siku, lakini sasa napika pakiti kati ya pakiti nne na sita kila siku,” anasema Masika, ambaye huuza chapati moja Sh10.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka kaunti ya Makueni, pia amepunguza kiasi cha kabeji anapika kutoka kabeji ya Sh100 hadi Sh30, maharagwe kutoka mikebe (gorogoro) minne hadi miwili na chai kutoka chupa mbili za chai (flaski) hadi moja.

Kabla ya kafyu kuanza, Masika, ambaye alisoma hadi darasa la nane katika Shule ya Msingi ya Kalawa, anasema alikuwa anafunga biashara yake saa nne usiku, lakini sasa anaharakisha kufunga kazi kabla ya saa kumi na mbili ili kafyu ikianze awe amefika kwake katika mtaa wa Baraka Mowlem.

Mambo yamebadilika kwa haraka kwa Masika, ambaye anasema hakuwahi kufahamu kafyu hiyo itamuathiri pakubwa hadi siku Machi 28 alipoanza kuona madhara yake. Siku hiyo, alipata hasara kubwa kwa kutopiga hesabu zake vizuri.

“Serikali ilipotangaza mambo ya kafyu, sikuchukulia kwa uzito; nilidhani ni mchezo tu. Baada ya kukosa kufungua biashara yangu Machi 27, nilirejea kwenye kibanda changu siku iliyofuata. Nilipika chapati 360, kabeji ya Sh100 na maharagwe kama kawaida pamoja na chai.

“Hata hivyo, ilipofika saa saba mchana, niligundua nilikuwa nimefanya makosa. Hali haikuwa nzuri kwa sababu wateja wangu, hasa wanaofanya kazi ya kujenga nyumba, hawakuonekana. Kumbe kafyu ilikuwa imepunguza muda wao wa kuwa kazini kwa hivyo waliona hakuna haja ya kutafuta chakula cha mchana. Siku hiyo, chakula kingi kilibaki.

“Sikuwa nimeuza chapati 48 nilipofunga siku, idadi ambayo sijawahi kushuhudia imebaki tangu nije hapa miaka miwili iliyopita. Pia, nililazimika kumwaga kabeji kwa sababu hakuna aliyekuwa amenunua.

“Nilibaki na chai flaski moja na maharagwe sufuria moja nzima. Kutoka hapo, nilishika adabu kuwa kafyu imeanza. Tangu wakati huo, nimepunguza vyakula ninavyopika,” anasema Masika, ambaye amefichua pia kuwa bei ya baadhi ya vitu anavyotumia katika biashara yake imepanda.

“Nimekuwa nikinunua pakiti moja ya unga kwa Sh120, lakini sasa ni Sh125. Mafuta ya kupika pia yamepanda kwa karibu Sh50,” anadai Masika, ambaye analipia kibanda chake Sh1,300 kila mwezi kutoka Sh1,000 alipoanza kukitumia.

Aidha, Masika ameshauri serikali jinsi ya kuzuia uenezaji wa virusi vya corona. Anapendekeza kuwa badala ya madaktari wote kusubiri wagonjwa wa virusi vya corona kwenye hospitali, waende mashinani na kupima kila mtu. “Mtu atakayepatikana na virusi hivyo, apelekwe hospitali kupokea matibabu hadi pale atakapopona,” anasema.