Habari Mseto

KAFYU: Kipigo cha mwaka Nakuru

March 28th, 2020 2 min read

Na SAMUEL BAYA

Wakazi wa Nakuru ambao hawakuwa wamefika nyumbani baada ya saa moja jioni Ijumaa walicharazwa viboko na polisi ambao walikuwa wakitekeleza amri ya kutotka nje.

Ijumaa jioni ilikuwa siku mbaya kwa wakazi ambao walijipata mikononi mwa polisi ambao hawakuwa na huruma na kuwacharaza viboko.

Wale wanjanja zaidi waliwakwepa polisi ila magari yao na pikipiki zao zilitandikwa na marungu ya maafisa hao ambao walikuwa wakitekeleza amri ya kutotoka nje usiku ambayo ilitangazwa Juamtano iliyopita na Rais Uhuru Kenyatta.

Wengi wa wale waliopata kichapo ni wale medereva wa malori ya masafa marefu ambao bila kuwa na habari walijipata katikati ya songobmwingo hilo.

Vurugu ilianza katika mzunguko wa barabara ya kuelekea Kabarak na ile barabara kuu wakati ambapo maafisa wa polisi waliweka mtego katika juhudi za kuwanasa wale waliokiuka agizo hilo.

Kizaazaa kilianza baada ya dereva mmoja ambaye alijulikana kama James alivyopjipata akipata kichapo cha nyahunyo kadhaa.

Unaitwa nani, polisi akamuuliza dereva huyo. Baada ya kujitambulisha, dereva huyo ambaye alikuwa akisafirisha beramu za lami kutoka jijini Mombasa alijipata akipokea kipigo kutoka kwa maafisa hao wa usalama.

“Wewe ni mkenya,” akahoji tena askari huyo huku afisa mwengine wa polisi akiendelea kumchapa viboko. Baadaye askari walimwagiza jamaa huyo kuingia  ndani ya gari na kuondoka lakini wakati huo wote, jamaa alikuwa amepata kichapo kikali kutoka kwa maafisa hao.

Naye mlinzi wa usiku ambaye alijifanya afisa wa usalama na hata kuandamana nao kwa muda katika barabara za jiji alipata kichapo cha mbwa baada ya askari hao kumgeuka.

Awali jamaa huyo alijipata mashakani baada ya polisi mmoja kumgundua kwamba alikuwa akirekodi video ya opereseheni yao wakiwatwanga wananchi.

“Wewe ni nani uko na sisi. Hebu toa simu mara moja,” akasema afisa huku jamaa akiendelea kupigwa viboko.

“Huyu ndiye ambaye amekuwa akiturekodi,” akasema afisa mmoja kando yake.

Baada ya kupigwa na kuachwa akichechemea, jamaa huyo aliambiwa akimbie kutoka eneo hilo.

“Kwenda kabisa wewe na usirudi eneo hili,” akasema polisi moja.

Katika mzungukuko huo huo wa Westside Mall, jamaa mmoja akipeleka gari dogo alipata kichapo cha mbwa koko baada ya kuhoji askari hao kwanini walikuwa wakimzuia kuendelea na safari.

Jamaa huyo ambaye alidai kuwa daktari aliwaambia maafisa wa usalama kwamba alikuwa ametoka kushughulikia mgonwja lakini hawakumsikia na badala yake wakaanza kumtandika vikali. Hali hiyo ilimlazimu jamaa huyo kuacha gari lake katikati ya barabara na kuwa ni mguu niponye.

Nje ya hoteli ya Merica, msimamzi wa kanda ya Bonde La Ufa George Natembeya alisistiza kwamba lazima watu waheshimu kafyu kama ilivyotangazwa na serikali.

Hata hivyo tulipomuuliza endapo alikuwa na habari kwamba watu walikuwa wakipigwa marungu na askari Bw Natembeya alisema kuwa kila mmoja anafaa kuheshimu sheria. Hakufafanua kuhusu kichapo ambacho kilikuwa kikiendelea karibu tu na mahali ambapo wananchi walikuwa wakipitia changamoto mbalimbali.

“Wakati tuliposema kwamba lazima watu wabakie nyumbani na kwamba ratiba yote ilikuwa imetolewa, hiyo ndiyo jambo ambalo lilifaa litekelezwe. Tunajua kwamba jambo kama hili likianza kunakuwa na changamoto lakini ukweli ni kuwa lazima watu wafie nyumbani mwa muda ambao unafaa wala sio vinginevyo,” akasema Bw Natembeya.