Kafyu kuendelea

Kafyu kuendelea

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amezidisha utekelezaji wa amri ya kafyu na masharti mengine ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19 hadi Machi 12, 2021, huku shule zikifunguliwa baada ya kufungwa Machi 15, 2020.

Alitoa agizo hilo kupitia amri kuu aliyoitoa Jumapili siku moja kabla ya wanafunzi kurejea shuleni kwa masomo ya kawaida.

“Ingawa kiwango cha maambukizi ya corona kinaendelea kushuka, janga hilo lingali tishio kubwa kwa sekta yetu ya afya na uwezo wetu wa kuzalisha mali. Kwa hivyo, kuna uwezekano kwamba maambukizi yanaweza kupanda kwa mara nyingine ndiposa masharti hayo ni muhimu kuendelea kuzingatiwa,” Rais Kenyatta akasema katika agizo hilo.

Hii ina maana raia watahitajika kusalia nyumbani kuanzia saa nne za usiku hadi zaa kumi alfajiri kila siku hadi Machi 12, 2020.

Masharti mengine ambayo Rais Kenyatta aliongeza muda wa kutekelezwa kwayo hadi Machi 12, 2021 ni kufungwa kwa baa na vilabu vya burudani kufikia saa tatu za usiku kila siku.

Vile vile, Rais Kenyatta alisema kuwa masharti yote kuhusu mikutano ya kidini na ibada makanisani na misikitini pia yataendelea kuzingatiwa.

“Masharti hayo yataendelea kuzingatiwa kulingana na kanuni zilizotangazwa Baraza la Viongozi wa Kidini kama zilivyoambatanishwa na masharti ya Wizara ya Afya kuhusu udhibiti wa kuenea kwa Covid-19,” Rais Kenyatta akasema.

Kiongozi wa taifa pia alisema kuwa masharti kuhusu idadi ya watu wanaoruhusiwa kuhudhuria hafla za harusi na mazishi itasalia iliyotangazwa mnamo Novemba 4, 2020.

Ni watu 200 pekee wanaoruhusiwa kuhudhuria hafla ya mazishi na harusi kama hatua ya kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Rais Kenyatta pia aliendeleza marufuku dhidi ya mikutano ya kisiasa na mikutano mingineyo ya hadhara.

Vile vile, kiongozi wa taifa aliagiza kuwa walimu wenye umri wa miaka 58 kwenda juu au wale wenye magonjwa sugu wafundishe kupitia mitandaoni au katika sehemu wazi.

“Kwa njia kama hii, watapunguza uwezekano wa walimu kama hao kuambukizwa virusi vya corona,” akasema Rais Kenyatta.

Rais pia alisema kuwa shule ni sharti zihakikishe kuwa zina vituo vya kutosha vya kuwawezesha wanafunzi kunawa mikono kulingana na masharti ya Wizara ya Afya.

Huku shule zikifunguliwa Jumatatu, Rais pia alisema shughuli za michezo zitasalia kupigwa marafuku. Vile vile, mashindano ya michezo ya kuigiza, nyimbo na hafla za kutoa zawadi zinazoshirikisha zaidi ya shule moja hazitaruhusiwa.

You can share this post!

Magoha atetea tena masomo ya chini ya miti

Leicester City wacharaza Newcastle United na kuingia ndani...