KAFYU: Pigo kwa wenye vilabu vya densi na makahaba

KAFYU: Pigo kwa wenye vilabu vya densi na makahaba

Na MISHI GONGO

WAMILIKI wa vilabu vya densi na makahaba wamepata pigo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza marufuku ya kufungwa kwa sehemu hizo kwa siko 30 zaidi.

Vilabu hivyo vilifungwa miezi sita iliyopita kufuatia kuzuka kwa ugonjwa hatari wa Covid-19.

Wengi wa wamiliki wa sehemu hizo walikuwa na matumaini ya kuruhusiwa kuendeleza biashara zao na kuondolewa marufuku ya kuzuia kutoka nje baada ya saa tatu usiku.

Mmiliki wa kilabu kimoja eneo la Bombolulu, Mombasa Bw Denis Irungu amesema tangu kuzuka kwa janga la corona biashara yake imedorara.

“Masharti mengi yamelegezwa kumaanisha kuwa ugonjwa umepungua hivyo nilikuwa na matumaini ya kurudia biashara yangu karibuni lakini sasa haiwezekani,” amesema.

Amesema kwa sasa anauza pombe mitandaoni japo havuni kama anavyovuna klabu ikiwa wazi.

“Kuna watu walikuwa wakikesha hapa lakini kwa sasa haiwezekani. Nilikuwa nauza pombe na nyama,” amesema.

Mwanamke mmoja ambaye anafanya biashara ya ngono – Taifa Leo haimtaji kumpa faragha – anasema wateja wamepungua kufuatia wengi kuhofia saa za kafyu kuanza kuwapata wakiwa nje.

“Ni ngumu kufanya biashara hii kwa sasa ambapo tunalazimika kukutana na wateja mchana. Wateja wetu wengi wako katika ndoa hivyo wanaona aibu kuonekana na hivyo biashara imezorota pakubwa,” amesema.

Wawili hao wamesema kufuatia hali hiyo, wamelazimika kutafuta njia mbadala za kujipatia riziki.

Mwanamke kahaba huyo anasema kwa sasa anafanya vibarua vya kufua nguo.

“Kufua kunahitaji muda na nguvu. Kwa siku nafulia watu wawili au watatu pekee ambapo kutoka kwa wateja hawa najipatia kati ya Sh600 au 800 ambazo ni kidogo sana ikilinganishwa na ukahaba,” amesema.

Katika hotuba yake Rais Kenyatta amewapongeza Wakenya walio zumbua shughuli zingine baada ya kazi zao za zamani kuathirika kwa njia hasi na janga la corona.

You can share this post!

Rais Kenyatta aamuru asasi za uchunguzi zitumie siku 21...

Sonko aruhusiwa kusuluhishia nje ya mahakama kesi ya...