Habari Mseto

KAFYU: Polisi na majambazi sasa wahangaisha Wakenya

March 31st, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VISA vya uhalifu vimeendelea kutekelezwa na polis pamoja na magenge hatari wakati wa kafyu inayotekelezwa na serikali kuepusha ueneaji virusi vya corona.

Katika kaunti ya Nakuru, mfanyabiashara mmoja analilia polisi baada ya duka lake kuvunjwa na maafisa hao waliokuwa wakitekeleza kafyu.

Kisa hicho kilitokea katika mtaa wa Top Ten, eneo la Langalanga viungani mwa mji wa Nakuru Jumamosi usiku.

Maafisa wakuu wa polisi wakiongozwa na kamanda wao katika kaunti hiyo Bw Stepehn Matu walisema hawakuwa na habari kuhusu tukio hilo.

Katika kaunti ya Uasin Gishu, polisi wanachunguza tukio ambapo walinzi wa kaunti na wale wa kibinafsi waliwavamia vijana wa kurandaranda mitaani na kuwajeruhi watatu Jumapili usiku Eldoret.

Jana, vijana hao walivamia kituo cha Central mjini humo wakitaka walinzi hao wakamatwe.

Katika kaunti ya Laikipia, mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 23 ulipatikana jana asubuhi mtaani Jua Kali mjini Nyahururu.

Polisi walisema mwili huo uliotambuliwa kuwa wa John Ngugi uliopatikana na mwanabodaboda ambaye alipiga ripoti kituoni cha polisi.

Nacho chama cha Madereva wa Kusafirisha Mizigo Nchini (KTA), kimeitaka serikali kuchukulia hatua kali maafisa wa polisi waliowapiga madereva wa kusafirisha bidhaa ambao walikuwa wameorodhoshwa kutoa huduma hata baada ya saa za kafyu kufika.

“Polisi hawafai kutumia nguvu nyingi wanapowakabili wananchi na hivyo wote waliohusika wanafaa kuchukuliwa hatua kali,” akasema Newton Wang’oo ambaye ni mwenyekiti wa KTA, katika taarifa.

Huko Siaya afisa wa polisi alikamatwa Jumamosi kwa kukataa kutii kafyu.Afisa huyo, Hussein Abdulahi, alipatikana katika baa akiburundika na wakazi mwendo wa saa mbili na nusu usiku.

Katika mtaa wa Witeithie Juja, Kaunti ya Kiambu, polisi walilazimika kuvunja maskani ya burudani ili kuwafurusha walevi waliokuwa wakijiburudisha na kinywaji baada kafyu kuanza.Ilidaiwa mmiliki wa maskani hiyo aliamua kuwafungia wateja wake ndani ya baa hiyo.

Ripoti za SAMUEL BAYA, DIANA MUTHEU, STEVEN NJUGUNA, LAWRENCE ONGARO, DENNIS LUBANGA, DICKENS WASONGA Na KALUME KAZUNGU