Kafyu: Raia kuumia zaidi vigogo wakieneza corona kijeuri

Kafyu: Raia kuumia zaidi vigogo wakieneza corona kijeuri

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA wanaotegemea biashara za usiku kujitafutia riziki wataendelea kuteseka baada ya serikali kuongeza muda wa kafyu kwa siku 30 zaidi.

Biashara kama vile kumbi za burudani na safari za usiku zimekwama tangu kuwekwa kwa kafyu kwa mara ya kwanza mnamo Aprili, mwaka 2020.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe jana alisema kuwa serikali itatumia kipindi hicho kuchanja idadi kubwa ya watu.

“Ili kufungua uchumi baada ya siku 30, ninawahimiza watu wengi kujitokeza kuchanjwa,” akasema Bw Kagwe alipokuwa akihutubu jijini Nairobi.

Bw Kagwe pia alisema kuwa marufuku ya kuandaa mikutano ya kisiasa itaendelea kwa siku 30 zaidi.

Agizo hilo la serikali limekuwa likivunjwa na wanasiasa wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wa Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga ambao wamekuwa wakihutubia umati wa maelfu ya watu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Serikali inaonekana kupuuza wito wa Wakenya ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kushinikiza Rais Kenyatta kuondoa kafyu ambayo imekuwa ikitekelezwa kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri.

Bw Kagwe alitangaza kuongezwa kwa muda wa kafyu, siku moja baada ya shirika la afya la Amref Africa kumtaka Rais Kenyatta kuondoa kafyu ili kufungua uchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Amref, Dkt Githinji Gitahi alihimiza serikali kuelekeza juhudi zake katika utoaji wa chanjo.

Jumatatu, Bw Kagwe alisema kuwa Kenya bado haijafikisha kiwango cha maambukizi kinachohitajika na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kufungua nchi.

Kulingana na mwongozo wa WHO, watu wanaopatikana na virusi vya corona ni sharti wawe chini ya asilimia nne ya wanaopimwa kwa siku katika muda wa siku 14 mfululizo kabla ya nchi kujitangaza kwamba imeshinda virusi vya corona.

“Tutaendelea kutekeleza masharti yaliyowekwa, kama vile kuhakikisha hakuna yeyote anayepaswa kuwa nje kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri,” akasema.

Waziri Kagwe alisema kuwa serikali iliafikia uamuzi huo kufuatia mashauriano yaliyofanyika kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kamati ya Kitaifa ya Kushughulikia Hali ya Corona nchini (NERC).

Kufikia sasa, baadhi ya sekta ambazo zimerejelea shughuli zake za kawaida ni ile ya uchukuzi, kwani magari yote ya usafiri yanawabeba abiria kama ilivyokuwa awali.

You can share this post!

ODONGO: Kanu ina kibarua kurejelea umaarufu wake wa awali

Maafisa 3 waliopuuza kumuachilia Kuria hatarini