Habari Mseto

KAFYU: Walevi wang'ang'ania pombe dakika za mwisho

March 28th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Makumi ya wanywaji wa vileo mtaani Kariobangi South walimiminika katika duka moja kama kwamba dunia ilikuwa ikiisha kabla ya kafyu kuanza kutekelezwa kote nchini Kenya ikinuiwa kuimarisha vita dhidi ya virusi hatari vya corona.

Duka halikuwa na shughuli nyingi kabla ya saa kumi na mbili jioni Ijumaa. Hata hivyo, ilipogonga saa kumi na mbili, wanywaji walifurika katika duka hilo kama nyuki mzingani.

Mmoja baada ya mwingine alionekana akitoka kwenye kaunta akibeba chupa ama mikebe kadhaa mikononi.

Walisikika wakisema kafyu imewaharibia ‘members day’ kwa sababu hawawezi kunywa nje ya duka hilo kama walivyokuwa wamezoea kila Ijumaa.

Hawakutaka kabisa kupigwa picha na walionya mwandishi huyu walipogundua alikuwa akitumia kamera ya simu yake kurekodi kilichokuwa kikuendelea.

Zikisalia dakika chache kafyu hiyo ianze saa moja kamili jioni, muuzaji wa vileo hivyo alifunga duka hilo mara moja na kuambia waliokuwa kwenye foleni wangefika kwenye duka hilo mapema kama kweli walikuwa na hamu ya kukata kiu.

Virusi hatari vya corona vimehangaisha dunia nzima ikiwemo Kenya, ambayo imeshuhudia visa 31 na mtu mmoja kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.