Habari

Kafyu ya mauti

April 1st, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

IDARA ya Polisi iliendelea kushutumiwa jana, baada ya mvulana wa miaka 13 kuongeza orodha ya watu waliodaiwa kuuawa na polisi wanaotekeleza kafyu kitaifa kuepusha usambazaji wa virusi vya corona tangu Ijumaa iliyopita.

Hayo yalitokea huku idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini ikifika 59.

Mwanafunzi huyo wa Darasa la Nane, Yasin Moyo, aliuliwa nyumbani kwao katika eneo la Kiamaiko, eneobunge la Mathare, Nairobi, Jumatatu jioni.

Moyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Ndururuno, alikuwa akicheza na ndugu zake katika baraza la nyumba yao kwenye ghorofa ya pili kabla ya kupigwa na risasi tumboni saa 1.00 jioni.

Familia yake imesisitiza kuwa mtoto wao alipigwa kimakusudi na polisi katili waliokuwa wakipiga doria.

“Daktari alituambia risasi iliingia tumboni ikampasua viungo muhimu vya ndani. Alieleza kwamba, mwanangu alivuja damu nyingi na walijaribu kila juhudi kumwokoa lakini akafariki kutokana na majeraha yake,” babake marehemu, Bw Hussein Moyo akaeleza.

Lakini polisi wanasema mvulana huyo alipigwa kimakosa na risasi iliyopoteza mwelekeo.

Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ilisema imeanzisha uchunguzi, ikiwemo kuchunguza risasi iliyomwangamiza mtoto huyo ili kubainisha bunduki iliyotumiwa.

Chama cha ODM kilitaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai abebeshwe msalaba wa maafisa katili.

Kupitia taarifa ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, chama cha ODM kilitaka Bw Mutyambai kuwajibikia kifo cha mvulana huyo.

“Inspekta Jenerali wa Polisi Bw Mutyambai ndiye anafaa kulaumiwa kwa mauaji ya Moyo. Polisi wanafaa kuzingatia haki za kibinadamu wanapotekeleza amri ya kutotoka nje,” akasema Bw Sifuna.

Visa vingine vya mauaji wakati wa kafyu vilikuwa vimeripotiwa katika Kaunti za Kwale, Siaya, Taita Taveta na eneo la Githurai, Kiambu ambako ilidaiwa wanaume watatu walifariki baada ya kupigwa na polisi.

Katika eneo la Voi, polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha kutatanisha cha mlinzi anayedaiwa kufariki kutokana na majeraha aliyopata baada ya kupigwa na maafisa wa usalama waliokuwa wakitekeleza amri ya kutotoka nje usiku.

Mwili wa mwendazake anayejulikana kama Kazungu, ulipatikana kwenye nyumba yake ya kupanga eneo la Maungu, katika barabara ya Nairobi-Mombasa.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti, Saidi Kiprotich alisema wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha mlinzi huyo.

Bw Kiprotich alisema kisa hicho tayari kimeripotiwa kwa Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA).

Katika eneo la Githurai, Kaunti ya Kiambu, wakazi waliandamana Jumapili wakitaka haki itendeke kwa mauaji ya watu watatu waliopatikana na majeraha ya kupigwa.

Wakazi wenye ghadhabu walikuwa wakiandamana na maiti ya mmoja wa waathiriwa kabla ya kutawanywa na polisi kwa vitoa machozi.

“Hakuuawa kwa risasi lakini alikuwa na majeraha kichwani na miguu na mikono yake ilikuwa imefura,” akasema mmoja wa waandamanaji hao.

Katika kisa cha Kwale, Mshirikishi wa Shughuli za Serikali katika Ukanda wa Pwani John Elungata jana alidai mhudumu wa boda boda, Hamisi Juma Idd, 49, hakuuliwa na polisi bali alipata ajali alipokuwa akitoroka polisi wakati wa kafyu Ijumaa.

Bw Elungata alisema mwendazake alipata ajali alipokuwa akijaribu kutoroka polisi.

“Tofauti na ripoti za vyombo vya habari, kisa hicho hakikutokea katika eneo la Likoni. Mwathiriwa alipata ajali alipokuwa akijaribu kukwepa polisi,” akasema.

Ripoti za Mary Wambui, Leonard Onyango, KNA na Fadhili Fredrick