Kafyu ya unyama

Kafyu ya unyama

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI imewashangaza Wakenya kuhusu busara ya kihayawani iliyotumia kulazimisha maelfu ya wakazi wa Nairobi kulala barabarani mnamo Jumamosi usiku.

Kulingana na busara ya serikali, hatua hiyo ilikusudiwa kuwa funzo kwa wanaojipata nje baada ya saa mbili za jioni, ambao ni wakati wa kuanza kwa kafyu maeneo ya Nairobi, Kiambu, Machakos, Nakuru na Kajiado.

Matokeo ya kufunga barabara yalikuwa ni wagonjwa kushindwa kufika hospitalini, na watoto wachanga pamoja na wazazi wao kulala kwenye baridi usiku kucha, hali ambayo yamkini ilichangia hata vifo.

Vizuizi hivyo viliwekwa katika Makutano ya Barabara ya Kayole, Uwanja wa Ndege wa Wilson, Barabara ya Lang’ata, Mwiki, Kasarani, Junction Mall, Hospitali ya Coptic, Arboteum, Ruai, Utawala, Duka la Two Rivers, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Barabara Kuu ya Thika.

Hata watoaji wa huduma muhimu wakiwemo madaktari, wauguzi, wanahabari na wasafirishaji wa vyakula hawakusazwa kwenye tukio hilo.

Ambulensi zilizokuwa zikisafirisha wagonjwa pia zilikatazwa kupita, na hivyo kuhatarisha maisha ya wengi, jambo ambalo serikali ilijitia hamnazo kulihusu.

Maafisa wa polisi waliokuwa kwenye vizuizi hivyo walisema walikuwa wameagizwa kwa amri kutoka juu kufunga barabara hizo na wasifungulie yeyote hata kama ni dharura kama ile ya ambulensi.

Kulingana na Msemaji wa Serikali, Cyrus Oguna, ilikuwa muhimu Wakenya kuonja mahangaiko hayo ili kuwalazimisha kuheshimu amri za kukabiliana na Covid-19.

“Kutii kanuni za kupunguza maambukizi ya Covid-19 kunahusisha kuheshimu saa za kafyu kuanzia saa mbili,” alisema Bw Oguna kwenye ujumbe.

Kauli yake ni kinaya kikuu kwani maafisa wakuu wa serikali wana sifa mbaya za kupuuza sheria, ikiwemo maagizo ya mahakama, tabia ambayo imeigwa na Wakenya wengine.

Katika Barabara Kuu ya Thika, wazazi waliokuwa wakipeleka mtoto wao hospitalini Gertrude walikwama huku mtoto wao akiendelea kuumia.

Waandishi wa Nation Media Group nao walijipata kwenye unyama wa serikali dhidi ya raia wake walipopata barabara zimefungwa na ikabidi wakae nje kwa muda mrefu usiku.

Katika mitandao ya kijamii, hasa Facebook na Twitter, Wakenya walieleza ghadhabu zao kuwa serikali imegeuka kuwa mnyanyasaji mkuu wa wananchi kwa kisingizio cha kutekeleza kafyu.

Wakenya walieleza ghadhabu zao kupitia hashitegi #UnlockOurCountry (Ifungue Nchi).

“Hii si busara. Huwezi kusababisha mgogoro ndipo utume ujumbe fulani. Hujali daktari ama muuguzi anayeenda kuhudumia wagonjwa hospitalini ama mtoto mchanga anayekimbizwa hospitalini,” akasema mwanauchumi Mohamed Wehliye.

“Hii ni njama iliyopangwa kimakusudi kuwatesa raia,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Sera na Kutatua Mizozo (ICPC), Ndung’u Wainaina.

Akasema Askofu JJ Gitahi wa Kanisa la Priesthood: “Kufungia watu barabarani walale huko si busara hata kidogo. Huwezi kutatua kosa kwa kutenda lingine.”

Licha ya malalamishi hayo, polisi jana walionekana kutobabaika, badala yake wakisema wataendelea kuhakikisha masharti ya kudhibiti virusi hivyo yamezingatiwa.

Kwenye taarifa, Mshirikishi Mkuu wa Nairobi, Bw James Kianda, alisema operesheni hiyo ilibaini Wakenya wengi wamekuwa wakikiuka kanuni hizo kimakusudi.

“Tulibaini Wakenya wengi huwa hawazingatii masharti kama kutokaribiana, kutozingatia saa za kafyu na kutovaa barakoa,” akasema.

Hata hivyo, alisema wataanza kutathmini upya operesheni zao ili kuhakikisha msongamano uliotokea katika Barabara ya Thika hautatokea tena.

Mwaka uliopita, polisi walilaumiwa kwa kutumia ukatili dhidi ya Wakenya, hali inayoonekana kujirudia licha ya ahadi za maafisa wakuu serikalini, wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

You can share this post!

MBWEMBWE: Bruno Fernandes si magoli tu pia kuunda pesa...

Kipchoge afagia NN Marathon, macho sasa kwa Olimpiki