Habari

Kafyu yasaidia kukabili magenge ya uhalifu Mombasa – Kamishna

September 7th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

KAFYU ya nyakati za usiku imetajwa kupunguza magenge ya uhalifu kama vile ‘Wakali Kwanza’ na ‘Wajukuu wa Bibi’ jijini Mombasa.

Kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo alisema tangu kuwekwa kwa marufuku visa vya magenge kuvamia wenyeji katika eneo la Kisauni na Likoni vimepungua.

“Marufuku yamefanya kazi ya mafisa wa polisi kuwa rahisi. Wakora ambao walikuwa wanajificha miongoni mwa watu wanatekeleza biashara usiku sasa haiwezekani,” akasema.

Akizungumza na Taifa Leo kamishna huyo alitaja kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa magenge hayo pia kama kulikosaidia kuwavunja makali wahalifu.

Alisema baadhi ya wahalifu waliuawa, kutiwa mbaroni huku wengine wakitoroka mji huo kwa kuhofia kukamatwa na maafisa wa polisi.

Alieleza kuwa hatua hiyo imechangia kupunguza pakubwa wahalifu ambao walikuwa wanahangaisha wenyeji wa jiji hilo.

Jiji la Mombasa lilikuwa linapambana na magenge ya ujambazi ambayo yalikuwa yanaongezeka kila uchao.

Mengi ya magenge hayo yalihusisha vijana wadogo wa kati ya umri wa miaka 15 hadi 25.