Kimataifa

Kagame na Museveni wakubali kujadiliana kuhusu mzozo

July 14th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

MARAIS Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda Ijumaa waliahidi kufanya mazungumzo kwa lengo la kusuluhisha tofauti za kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.

Viongozi hao walitoa ahadi hiyo walipokuwa katika kongamano kuhusu masuala ya usalama, ambalo liliandaliwa nchini Angola na Rais Joao Lourenco.

Lourenco alikuwa amemwalika Rais wa DR Congo Felix Tshisekedi katika kongamano hilo lililoandaliwa jijini Luanda vilevile.

Ujumbe uliosomwa baada ya majadiliano katika kongamano ulisema Rwanda na Uganda sasa ziko tayari kufanya mazungumzo, ili kusuluhisha matatizo ambayo yamekuwapo kwa miezi kadha iliyopita.

“Kongamano limekubali uamuzi wa Rwanda na Uganda kuendeleza mazungumzo kwa lengo la kutafuta suluhisho kwa matatizo yaliyopo,” ujumbe uliosomwa baada ya kongamano ukasema.

Hata kabla ya kongamano kuanza, Rais Lourenco alikuwa ameeleza kuwa baadhi ya masuala ambayo yangejadiliwa ni kufuatilia hali inavyoendelea baada ya mkutano ulioandaliwa Kinshasa mnamo Mei 31, kati ya DR Congo, Rwanda na Angola kuhusu hali ya usalama katika mipaka ya mataifa hayo matatu.

“Tulielewana kuwa mkutano mwingine utaandaliwa Luanda, Angola na pia tukakubaliana kumualika Rais Museveni kuungana nasi katika mkutano huu,” Rais Lourenco akasema.

Alisema kuwa ajenda ya mkutano wa awali ilikuwa kujadili masuala ya usalama baina ya mataifa hayo matatu, lakini suala la uhusiano baina ya Uganda na Rwanda likaongezwa.

Baada ya mkutano wa Jumamosi, waziri wa masuala ya nje wa Angola Manuel Domingos alisema kuwa mataifa hayo manne yalikubaliana kuwa Uganda na Rwanda wanafaa kuelewana.

“Kuhusu suala la uhusiano baina ya Rwanda na Uganda, makubaliano yamewekwa kuwa kutokana na kujitolea kwa mataifa hayo mawili kuendelea na mazungumzo ili kutafuta suluhisho kwa tatizo lililopo, mataifa hayo yaendelee kuzungumza,” akasema Domingos.

Aidha, Angola ilipewa kazi ya kufadhili mazungumzo baina ya Uganda na Rwanda, huku ikisaidiwa na DR Congo.

Kagame na Museveni wamekuwa wakijibizana hadharani kwa miezi kadha, kila mmoja akilaumu mwenzake kuwa anaingilia uongozi wa mwingine na kuchukua habari za kijasusi bila idhini.

Tofauti baina yao zimeathiri biashara tangu Februari, wakati Rwanda ilifunga mpaka kati yake na Uganda, hatua ambayo iliathiri biashara ya mataifa yote mawili.

Mnamo Mei, polisi wa Uganda walilaumu wanajeshi wa Rwanda kuwa waliingia nchini humo (Uganda) na wakaua watu wawili, madai ambayo Rwanda ilipinga.