Kagwe atishia kuadhibu walipishao chanjo

Kagwe atishia kuadhibu walipishao chanjo

Na WINNIE ONYANDO

WAZIRI wa Afya, Mutahi Kagwe ametishia kuyaondoa kwenye orodha majina ya vituo vya afya vyenye mazoea ya kuwatoza wananchi chanjo ya corona.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi kuhusu hali ya corona nchini, Bw Kagwe alisema majina ya vituo hivyo yataondolewa mara moja kwenye orodha ya vinavyotoa huduma za afya nchini.

“Ukienda hospitalini na udaiwe pesa ya chanjo, kubali kuchanjwa ila ukatae kulipa. Serikali inatoa chanjo bure. Watu kama hao wanaozidi kuwakandamiza raia watachukuliwa hatua,” akaonya Bw Kagwe.

Alisema serikali inatumia mabilioni ya pesa kuhakikisha kuna chanjo ya kutosha kwa wananchi wote. “Chanjo ni haki ya kila mmoja. Kila kituo cha afya lazima kitoe chanjo bure bila malipo kwa kila mmoja,” akasisitiza Bw Kagwe.

Waziri huyo alisema kuwekuwa na ripoti za madaktari wanaotembea mtaani bila mavazi rasmi na kuwachanja raia.Alisema madaktari kama hao pia wanajiweka katika hatari ya kupoteza kazi yao.

“Madaktari au maafisa wa afya wanaotembea mtaani wakitoa chanjo bila mavazi rasmi au beji za hudumu watachukuliwa kama matapeli. Tumepata ripoti kuwa kuna watu wanaovalia suruali aina ya jeans wakitoa chanjo kwa raia. Watu kama hao hawafai kutoa chanjo,” akaongeza Bw Kagwe.

Kutokana na hayo, Bw Kagwe alielekeza Chama cha Madaktari na Baraza la Madaktari wa Meno kuviondoa kwenye orodha vituo vyote vya afya vinavyotoza pesa kwa chanjo za corona.

Alisema kila kituo cha afya lazima kitoe ripoti kila wiki kuhusu matumizi ya dozi zote za chanjo ya corona huku akionya kuwa kituo chochote kitakachoshindwa kufanya hivyo kitaondolewa orodhani.

Kadhalika, waziri huyo alisisitiza kuwa hakuna chanjo inayopaswa kutolewa nje ya vituo maalumu vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.

“Kuna vituo maalum vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya ili kutoa chanjo. Vituo hivyo vina maafisa wa afya waliopata mafunzo maalum ya namna ya kutoa chanjo. Kama mwananchi, hakikisha kuwa unapata chanjo katika vituo hivyo,” akasema Bw Kagwe.

Hata hivyo, aliwahimiza wananchi wawe waangalifu na kuhakikisha kuwa wamepata chanjo. Kulingana na ripoti ya wizara ya Afya, nchi imetumia dozi zaidi ya 2.8 milioni kuwachanja raia.

You can share this post!

Wataka fidia iwepo viumbebahari wakiwajeruhi

Mgomo wa wahadhiri wasitishwa kupisha mashauriano ya...