Kagwe awaharibia Wakenya Krismasi

Kagwe awaharibia Wakenya Krismasi

Na WINNIE ATIENO

WADAU katika sekta zinazotegemewa sana kwa sherehe za kufunga mwaka, wanahofia kupata hasara Desemba ikiwa serikali itatekeleza agizo kuwa ni sharti kila mwananchi awe amepokea chanjo ydhidi ya virusi vya corona.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, aliagiza kuwa wananchi ambao hawajapokea chanjo hiyo wanyimwe huduma muhimu kama vile za serikali, uchukuzi, kuvinjari hotelini na vilabuni, miongoni mwa nyingine.

Wadau wa sekta ya utalii wamefichua kuwa baadhi ya wageni waliotarajiwa kuwasili kutoka maeneo mbalimbali nchini na kimataifa kwa shamrashamra za Desemba wameanza kufutilia mbali mipango yao kufuatia agizo hilo.

Wakuu wa hoteli walisema agizo hilo ni hatari na linaweza kusambaratisha biashara zao zilizokuwa zimeanza kufufuka.

Wasiwasi sawa na huo ulitolewa na wawekezaji katika sekta ya uchukuzi wa umma.

Sekta hizo ni miongoni mwa zilizopata pigo kuu tangu janga la Covid-19 lilipotangazwa nchini mwaka uliopita.

“Agizo hilo linatolewa wakati mbaya mno kwani huu ni msimu mkuu wa utalii. Inamaanisha Wakenya wengi wataonelea ni heri wasisafiri,” Mkurugenzi wa kampuni ya kitalii ya Pollman’s, Bw Mohamed Hersi, akasema.

Mapema mwezi huu wa Novemba, wadau katika sekta hiyo walisema wameanza kupokea idadi kubwa ya wageni baada ya masharti mengi yaliyokuwepo ya kuepusha Covid-19 kuondolewa baada ya maambukizi kupungua.

Wafanyabiashara walitarajia kuwa hali hiyo iliashiria msimu huu mkuu wa utalii ungewasaidia kufidia hasara walizopoteza tangu mwaka 2020.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi walikuwa tayari wameanza kujiandaa kwa sherehe na safari ambazo wamezitamani sana kwa miezi mingi.

Hata hivyo, baadhi ya wadau walisema hawatatii agizo hilo la serikali kwani, kwa mtazamo wao, watakuwa wanadhulumiwa haki zao kibiashara.

“Mbona wanataka kutuadhibu? Tangu Covid-19 ilipotokea, baadhi ya sera zinazotangazwa zimekuwa zikiathiri sana sekta ya utalii. Sisi tuko tayari kwa biashara na tunaomba tuwezeshwe kupata riziki,” akasema afisa wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli nchini, Dkt Sam Ikwaye.

Hata hivyo, Dkt Ikwaye alisema hawana pingamizi kuhusu hitaji la wananchi kupokea chanjo ila mbinu inayotumiwa na serikali ndiyo ni hatari kwa uchumi wa nchi.

Wadau hao walilalamika kuwa kila wakati mikakati inapowekwa katika vita dhidi ya Covid-19, sekta za kibiashara kama vile hoteli na uchukuzi wa umma barabarani ndizo hulengwa.

Kulingana nao, matokeo huwa ni kwamba biashara hizo ambazo huajiri mamilioni ya watu hupata hasara na hivyo basi kulazimika kutimua baadhi ya wafanyakazi wao au kuwapunguzia mishahara.

Walikosoa hatua hizi hasa ikizingatiwa jinsi mikutano ya hadhara ya kisiasa hukubaliwa kuendelea katika kila pembe ya nchi wakati ambapo sehemu za biashara huambiwa kufuata kanuni kali za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

“Mbona wanachukulia kuwa umati wa watu 300 hotelini au 40 katika mkahawa au 14 ndani ya matatu wana uwezo mkubwa wa kusambaza Covid-19 kuliko wale wote wanaohudhuria mikutano ya kisiasa kila mahali?” akauliza Bw Hersi.

Haya yamejiri siku chache baada ya Chama cha Wahudumu wa Matibabu, Wanafamasia na Madaktari wa Meno nchini (KMPDU) kukashifu serikali kwa kujifanyia maamuzi bila kushauriana na wadu wengine muhimu.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Davji Bhimji, alisema kulazimisha wananchi kupokea chanjo inaweza kusababisha wengi zaidi kuiepuka kwani watatilia shaka nia ya serikali.

Kulingana na Dkt Bhimji, serikali ingejituma zaidi kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo na pia kufanya iwe rahisi kwao kupokea chanjo hizo badala ya kutumia vitisho.

“Ni lazima wananchi washawishiwe kuhusu umuhimu wa chanjo kabla kuwalazimisha kuipokea. Badala ya kuzuia watu kuingia katika sehemu za burudani na kwingineko, mbona kusiwe na vituo vya chanjo katika sehemu hizo ili wale wanaotaka kuingia na hawajachanjwa, wapate njia rahisi ya kupokea chanjo?” akauliza.

Baadhi ya wadau katika sekta ya uchukuzi pia waliapa kutotii agizo hilo la serikali, wakisema kuwa biashara zao zitaathirika sana.

You can share this post!

STEVE ITELA: Hatua ya jeshi kusimamia mashirika isiwe fursa...

Tabitha aidhinishwa na wazee kuwania wadhifa wa seneta

T L