Bambika

Kagwe Mungai: Wanaoponda mahusiano yangu ya kimapenzi, kazi wanayo

May 8th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

MAHUSIANO ya kimapenzi baina ya maceleb huwa sawa na kuubeba mzigo wa mwiba kwani muda wote, huwa hawakosi kuchambwa na wafuasi.

Kapo moja ambayo kwa sasa imekuwa ikipondwa sana ni ya staa wa muziki Kagwe Mungai na boo wake muundaji maudhui Sharon Mwangi.

Wapenzi hao wamekuwa kwenye mahusiano kwa mwaka mmoja sasa na katika kipindi hicho, wamekuwa wepesi sana kupenda kuposti wakionyesha jinsi wanavyofurahia penzi lao.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wamehoji kuwa ni muda tu kabla mdudu uingie kwenye penzi lao kwani mara nyingi, kumeshuhudiwa mahusiano ya mastaa yakivunjika baada ya muda mfupi.

Kagwe kakiri kwamba kweli wanaishi kupambana na presha ya kuchambwa na mashabiki wao, ambao idadi yao kubwa imegeuka kuwa wakosoaji.

Hata hivyo, Kagwe anasema ametia nta masikioni na wala hakosi usingizi wake akiwaza wanachosema watu kuhusu penzi lake jipya.

“Wajua unapokuwa na mpenzi, huyo ni mtu ambaye yupo kwenye timu yako. Na mtu anapokuwa katika timu yako, vita vyake vinakuwa ni vita ya kwako. Ushindi wake unakuwa ni ushindi wako. Hili ni jambo ambalo mimi na yeye (Sharon) tunaishi kukumbushana na kwa kweli sijali wanachotaka kusema watu. La muhimu kwangu ni kumwona (Sharon) akiwa mwenye furaha muda wote. Yaani raha yangu ni kuona dimpo za kwake ziking’aa, mengine yote wala hayanijalishi wala kunivurugia Amani,” Kagwe kasisitiza.

Kwa wanaokesha kuponda mahusiano yao, basi kazi wanayo.

“Mimi nguvu zote nimezielekeza kuhakikisha mpenzi wangu ana furaha muda wote. Hili ndilo la muhimu kwangu,” akasema.

Mwaka 2023, kabla ya kuweka wazi kuwa wanadeti, Sharon alifichua kwamba, awali alitamani sana kuyafanya mahusiano yake kuwa ya kimya kimya lakini swahiba wake Joan akamshauri kuyaweka wazi endapo alikuwa anahisi kufanya hivyo.

Kuhusu kauli maarufu kutoka kwa wakosoaji wao ya “mtaachana tu” Sharon alisisitiza kuwa, haimjalishi sana na badala yake, anawaza zaidi kuyafurahia mahusiano yake kwa sasa, ambayo yanamwendea fiti.