Habari Mseto

KAGWE: Serikali Tanzania iwashughulikie raia wake wagonjwa wa Covid-19

May 20th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya ilisema Jumanne ni wajibu wa serikali ya nchi jirani ya Tanzania kushughulikia raia wake waliopatikana na ugonjwa wa Covid-19 maeneo ya mipakani.

Mikakati ya kuzuia msambao wa virusi vya corona maeneo ya mipakani inaendelea kuimarishwa, amri ya Rais Uhuru Kenyatta ya kufungwa kwa mipaka baina ya Kenya na Tanzania na vilevile Somalia, ikitekelezwa.

Rais alisema malori ya mizigo pekee ndiyo yataruhusiwa kuingia nchini.

Alichukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la visa vya Covid-19 miongoni mwa madereva wanaotoka katika mataifa hayo kuingia nchini na pia wanaopitia njia za mkato.

Ni hatua inayoonekana kupokea upinzani kutoka kwa taifa la Tanzania na kuzua tumbojoto, nchi hiyo ikipiga marufuku madereva wa Kenya kuingia humo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Jumanne matarajio yake ni kwamba Tanzania inashughulikie raia wake wagonjwa wake wa Covid-19, akieleza kwamba ni jukumu lao kama serikali.

“Tanzania itashughulikia raia wake. Sisi kama maafisa wa afya hatuwezi; kazi yetu ni kuwataarifu,” akasema.

Bw Kagwe alisema madereva wa taifa hilo waliopatikana na virusi vya corona maeneo ya mipakani wamerejeshwa nchini humo.

“Tunawarudishia watu wao, wajue watakavyowatibu. Ni jukumu lao kuwafuata. Wasipofanya hivyo, wao ndio wataumia,” akaonya.

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, wiki kadhaa zilizopita alinukuliwa akitilia shaka vifaa vya kukagua na kupima Covid-19.

Kisa cha kwanza cha ugonjwa huu kiliripotiwa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019.

Licha ya uhusiano wa Kenya na Tanzania kuonekana kudorora kufuatia visa vya Covid-19 mipakani, waziri alisema mataifa haya mawili yangali ‘ndugu’ na kwamba yataendelea kushirikiana.

Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kushirikiana ili kusaidia kuzuia maambukizi zaidi ya corona.