Michezo

Kahata asherehekea timu yake ya Simba ikiibuka bingwa wa Ligi Kuu Tanzania

June 29th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KIUNGO Mkenya Francis Kahata alishinda Ligi Kuu Bara katika msimu wake wa kwanza na Simba SC baada ya timu hiyo kufungua mwanya wa alama 19 juu ya jedwali ambao hauwezi kuzibwa na nambari mbili Young Africans.

Kahata alijiunga na Simba hapo Julai 4, 2019 akitokea Gor Mahia aliyokuwa ameisaidia kufagia mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya.

Mchezaji huyo, ambaye pia aliwahi kuchezea Thika United (Kenya), University of Pretoria (Afrika Kusini) na KF Tirana (Albania), hakutumiwa na kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck dhidi ya Tanzania Prisons hapo Juni 28.

Hata hivyo, Simba ilipata pointi moja muhimu iliyohitaji kutwaa taji ilipolazimisha sare ya 0-0 dhidi ya wenyeji hao wao na kufikisha alama 79 kutokana na kusakata mechi 32 kwenye ligi hiyo ya timu 20.

Matokeo hayo yalitosha kuzima matumaini madogo mahasimu wao wa tangu jadi Yanga walikuwa nayo. Mabingwa mara 22 Yanga, ambao wameajiri kipa Mkenya Farouk Shikalo, walipepeta Ndanda 3-2 Juni 27 na kufikisha jumla ya alama 60. Simba, ambayo imepata mabao yake mengi kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Gor, raia wa Rwanda Meddie Kagere (20), inajivunia kushinda ligi hiyo kwa mara 21 sasa.

Azam (alama 59), Namungo (56), Coastal Union (48), Polisi Tanzania (47), JKT Tanzania (47), Kagera Sugar (45), Biashara Mara United inayonolewa na kocha Mkenya Francis Baraza (44) na Tanzania Prisons (43) zinakamilisha orodha ya timu 10 za kwanza kwenye ligi ya msimu huu iliyoanza Agosti 29, 2019.