Michezo

Kahawa Queens mtindo ni kugawa dozi

July 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kahawa Queens iliendeleza mtindo wa kugawa dozi dhidi ya wapinzani wao kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza baada ya kuvuna alama sita muhimu uwanjani Kahawa Barracks, Nairobi.

Vipusa hao wa kocha, Joseph Wambua walizamisha Mombasa Olympic kwa mabao 6-0 kabla kulaza Sunderland Samba FC bao 1-0.

Kahawa Queens inayoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza ilinasa ufanisi huo kupitia Jentrix Kuyudi na Lucy Mukhwana waliofunga mabao mawili kila mmoja, huku Patricia Amaase, Emily Auma na Dorcas Awuor kila mmoja akiitingia bao moja.

”Nashukuru wachezaji wangu kwa kazi njema wanaofanya tayari wameonyesha wanapania makubwa,” kocha huyo wa Kahawa Queens alisema na kuongeza kwamba wanafahamu kutangulia siyo kufika.

Naye Wilyckister Shimwati alicheka na wavu mara moja na kubeba Mukuru Talent Academy kuzaba Limuru Starlets bao 1-0 katika Uwanja wa Shule ya Upili ya Embakasi Girls, Mukuru Embakasi, Nairobi. Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Moving The Goalpost (MTG) United ilituzwa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Joy Love FC kuingia mitini.

Kufuatia matokeo hayo, Kahawa Queens ingali kileleni kwa kuzoa alama 24 baada ya kushinda mechi zote nane ilizocheza. MTG ilirukia nafasi ya pili kwa kufikisha alama 13 sawa na Sunderland Samba tofauti ikiwa idadi ya mabao.