Michezo

Kahawa Queens wafunga kazi kwa kuigaragaza MTG 4-1

September 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kahawa Queens ilikamilisha kampeni zake kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza kiume baada ya kuponda Moving The Goalpost (MGT) United kwa magoli 4-1 uwanjani MTG Mjini Mombasa.

Naye mchana nyavu Lorenita Lupemba alitikisa wavu mara moja na kusaidia Mukuru Talent Academy kuvuna ufanisi wa goli 1-0 dhidi ya Joy Love FC na kuibuka ya tatu kwenye jedwali kwa alama 20, sawa na Mombasa Olympic FC.

Warembo hao chini ya kocha, Joseph Wambua mwanza walishusha mechi safi wakidhamiria kukunja kampeni za kipute hicho bila kushindwa.

Wacheza hao walitimiza azimio lao walipochuna ufanisi huo kupitia juhudi zake Everline Juma, Jentrix Kuyudi, Lucy Mukhwana na Emmy Kante kila mmoja alipopiga kombora moja safi.

”Kusema kweli tunashukuru wachezaji wangu kwa kazi njema waliofanya dhidi ya wapinzani wetu huku tukijivunia kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu msimu ujao,” alisema nahodha wa Kahawa, Dorcas Owuor.

Nahodha wa Mukuru Talent Academy, Wilkister Shimwati akizungumza na wenzake kabla ya kuingia mzigoni kukabili Joy Love FC kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza katika Uwanja wa Shule ya Embakasi Girls, Mukuru Kwa Njenga, Nairobi. Mukuru Talent Academy ilishinda goli 1-0. Picha/ John Kimwere

Nao wachezaji wa kikosi cha Sunderland Samba FC walishindwa ujanja na kukubali kulala kwa bao 1-0 mbele ya wenyeji wao Soccer Sisters. Itakumbukwa Sunderland Samba ilifungua kampeni zake kwa kishindo na kuonyesha dalili za kubeba taji la muhula huu.

Hata hivyo waliteleza walipondwa na Kahawa Queens kwenye mechi za mkumbo wa kwanza ambapo hatimaye walimaliza nne bora kwa alama 18, mbili ya Soccer Sisters.

Licha ya Kahawa kushiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza ilifaulu kuzipiga timu zingine kwa zaidi ya magoli matano ila Mukuru Talent iliponea. Mukuru chini ya nahodha, Wilkister Shimwati iliibuka timu ya pekee kupigwa kwa mabao machache kwenye mechi zote mbili (nyumbani na ugenini).

Timu ilishindwa kwa jumla ya mabao 3-0 ambapo kwenye mkumbo wa kwanza ililazwa mabao 2-0 kisha kwenye patashika ya marudiano ilizabwa goli 1-0. Nayo MTG United ilipondwa kwa magoli 4-0 ugenini kisha katika ardhi ya nyumbani ililimwa mabao 4-1.