Michezo

Kahawa Queens wafuzu kushiriki Ligi Kuu

August 12th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa kikosi cha Kahawa Queens wameketi mkao wa subira kutawazwa malkia wa michezo ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza na kupokezwa cheti cha kupanda ngazi kucheza gozi ya Ligi Kuu muhula ujao.

Warembo hao walizoa ufanisi huo huku wakiwa wamebakisha patashika tatu kukamilisha ratiba yao walipobugiza Limuru Starlets magoli 7-0 Ugani St Pauls University, Limuru.

Naye Kaluwa Pascal alitikisa wavu mara mbili na kubeba Moving the GoalPost (MTG) United kulima Sunderland Samba mabao 2-0 na kujiongezea tumaini la kuibuka ya pili.

Kahawa Queens ya kocha, Joseph Wambua Mwanza ilinasa ufanisi huo kupitia Jentrix Kuyudi alipotikisa wavu mara nne, Lucy Mukhwana aliyepiga kombora mbili safi huku Patricia Amaase akiitingia bao moja.

Kocha wa Kahawa Queens, Joseph Wambua Mwanza abebwa baada ya kikosi hicho kuthibitishwa kimetwaa tikiti ya kushiriki soka ya Ligi Kuu ya wanawake msimu ujao. Picha/ John Kimwere

Kahawa imewafungia wapinzani wao kwa kufikisha pointi 33 ambapo hata MTG United ikishinda mechi zake tatu itafikisha alama 31. ”Nashukuru vigoli wangu wote kwa kazi njema waliofanya maana kipute cha daraja la kwanza tumeshiriki mara moja na kufaulu kusonga mbele,” kocha Mwanza alisema.

Kahawa ilitwaa mafanikio hayo baada ya kushinda mechi zote 11 ambazo imecheza huku ikifuma kimiani magoli 41 na kufungwa mabao mawili.

Nayo Mombasa Olympic ilirejea makwao kwa tabasamu ikijivunia kurarua Joy Love FC kwa magoli 7-0 kisha kubeba goli 1-0 mbele ya Mukuru Talent Academy. Kwa mara nyingine, Joy Love FC iliachia alama tatu muhimu ilipolazwa magoli 6-0 na Soccer Sisters.

Warembo wa Kahawa Queens na wafausi wao wakisherekea baada ya kuthibitishwa kunasa tikiti ya ya kushiriki soka ya Ligi Kuu ya wanawake. Picha/ John Kimwere

Kocha wa Kahawa Queens akizungumza na Taifaleo Dijitali aliwapongeza Neddy Atieno, Christine Wekesa, Everline Étoo’Juma na Emily Auma kwa kuibuka mstari wa mbele kuwaandalia wenzao pasi safi ili kufunga. Pia alitoa pongezi zake kwa safu ya uvamizi ikiongozwa na Patricia Amaase, Lucy Mukhwana na Jentrix Kuyudi kwa kuonyesha kazi nzuri katika kila mechi.

Kadhalika alisema ,’Nahodha wangu Dorcus Awuor namshukuru sana amekuwa akiongoza safu ya difensi vizuri hali iliyochangia kufungwa mabao mawili pekee.”

Katika safu hiyo nahodha huyo amekuwa akishirikiana nao Margaret Atieno, Joan Naututu bila kumsahau mlinda lango wao Maureen Shimuli Bukaya.