Michezo

Kahawa Queens wanusia ubingwa

August 5th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TUMAINI la Limuru Starlets kuandikisha angalau ushindi wa kwanza msimu huu kwenye mechi za Kundi A, Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza liligonga mwamba ilipoyeyusha alama sita sita muhimu baada ya kusakata patashika mbili ugenini katika Kaunti ya Mombasa.

Nao warembo wa Kahawa Queens waliendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao waliporarua Soccer Sisters kwa magoli 3-0 Uwanjani Kahawa Barracks, Nairobi.

Limuru Starlets ya kocha, James Kairu iliona giza ilipokung’utwa mabao 4-3 na Moving The Goalpost (MTG) kisha kudungwa bao 1-0 na Mombasa Olympic FC. Kwenye matokeo hayo, Sunderland Samba ilishindwa kufana katika ardhi ya nyumbani ilipoagana sare tasa na Mukuru Talent Academy Uwanjani KNH, Nairobi.

Kahawa Queens ya kocha, Joseph Wambua Mwanza iliandikisha mchezo wa kumi bila kupoteza na kujiweka pazuri kutwaa ubingwa wa taji hilo pia kujikatia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya (KWPL) msimu ujao.

Vigoli hao waliteremsha soka safi na kuzoa ufanisi huo kupitia Patricia Amaase aliyetikisa wavu mara mbili huku Neddy Atieno akipiga kombora moja safi.

”Bila kupapasa macho na kule napongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri pia nawaambia shughuli bado,” kocha huyo wa Kahawa alisema na kuongeza kuwa hawawezi kusherekea maana mpira hauna heshima. Nayo MTG iliendelea kusalia katika nafasi ya pili kutokana na magoli ya Dorcas Ndombi aliyepiga ‘Hat trick’ naye Mwanaidi Karisa aliifungia bao moja.

Kwenye jedwali, Kahawa Queens ambayo ndiyo mwanzo kushiriki kipute hicho ingali kifua mbele kwa kuzoa alama 30, 11 mbele ya MTG baada ya kila moja kucheza mechi kumi. Kahawa ambayo imebakisha mechi nne kukamilisha ratiba ya kampeni za kipute hicho msimu huu inahitaji kushinda mechi moja pekee ili kutwaa taji hilo mapema.

Kulingana na msimamo huo Kahawa ikishinda mechi hata MTG ikishinda mechi zake nne zilizobaki kamwe haiwezi kuwapiku vipusa hao.

Kahawa ikijiongezea ushindi mmoja itafikisha pointi 33, nayo MTG ikishinda mechi zote nne itakusanya alama 31. Wachezaji wa Sunderland Samba wamefunga tatu bora kwa kuvuna alama 16, mbili mbele ya Mukuru Talent Academy.