Michezo

Kahawa Queens wararua Mombasa Olympic tena

July 31st, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kahawa Queens iliendelea kutesa washiriki wengine baada ya kuandikisha ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Mombasa Olympic kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza iliyochezewa uwanjani wa Lasco Ziwani mjini Mombasa.

Nao wasichana wa Sunderland Samba walicharaza JoyLove FC kwa magoli 4-0 wakati Moving The Goalpost (MTG) United ikizoa goli 1-0 mbele ya Mukuru Talent Academy. Kahawa Queens iliingia mzigoni ikijivunia kutandika wenyeji hao magoli 6-0 kwenye mechi ya mkumbo wa kwanza iliyochezewa jijini Nairobi.

Vipusa wa Kahawa chini ya kocha, Joseph Wambua Mwanza walishuka dimbani kwa kusudi moja kutesa na kuvuna pointi zote muhimu.

Kikosi hicho kilitwaa ushindi huo kupitia Everline Juma na Lucy Mukhwana waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

”Napongeza wachezaji wangu kwa kazi njema waliofanya kwenye mchezo huo ingawa uwanja ulikuwa mbovu,” kocha wa Kahawa alisema na kuongeza kuwa wanalenga kuendeleza mtindo huo kwenye mechi sijazo.

Nayo Sunderland Samba ilirukia tatu bora kwa kufikisha alama 15 baada ya Sylvia Akoth kufuma kimiani magoli matatu huku Irene Aluoch ikiitingia bao moja.

Kwenye mfululizo wa ngarambe hiyo, Limuru Starlets ilijituma kiume na kulazimisha sare tasa dhidi ya Soccer Sisters. Kufuatia matokeo hayo, Kahawa Queens ingali kileleni kwa alama 27 baada ya kusakata mechi tisa na kushinda zote. Nayo MTG imezoa alama 16 na kufunga mbili bora.