Michezo

Kahawa Queens wazidi kudhihirisha makali yao

June 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kahawa Queens iliendeleza mtindo wake kutembeza vipigo mbele yua wapinzani wao kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza baada ya kuchoma Joy Love mabao 5-0 uwanjani Kahawa Barracks, Nairobi.

Vipusa hao ambao hutiwa makali na kocha, Joseph Wambua walishusha mchezo safi wakilenga kutesa wapinzani wao na kuwafanya kuondoka mikono mitupu bila alama wala goli hata moja.

Katika mpango mzima waliingia mjegoni kupiga shughuli za kweli wakilenga kuendeleza mtindo wa kugawa gozi dhidi ya wapinzani wao. Walitimiza azimio lao kupitia Margaret Atieno, Christine Wekesa, Lucy Mukhwana, Patricia Amaase na Jentrix Kuyudi baada ya kila mmoja kucheka na wavu mara moja.

Kikosi hicho ambacho ndiyo mwanzo kushiriki ngarambe hiyo kimeanza kuogopwa maana kimeonyesha ujio wa kasi.

”Tuna mchezo mmoja kapuni dhidi ya Mombasa Olympic tutakaocheza kwenye ufunguzi wa mechi za mkumbo wa pili,” kocha wa huyo wa Kahawa Queens alisema huku akishukuru wachezaji wake kwa kazi nzuri, pia alishukuru wafuasi wao na wasimamizi wao kwa kuwapa sapoti kwenye kampeni za kinyang’anyiro cha msimu huu.

Wasichana wa Kahawa Queens ambao husakata gozi kama wanaume chini ya nahodha, Neddy Atieno wangali kifua mbele kwa kukusanya alama 18, sita mbele ya Sunderland Samba FC baada ya kusakata patashika sita na saba mtawalia.