Michezo

Kahawa Queens wazidi kufunza wapinzani gozi

August 28th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KWA mara nyingine wasichana wa Joy Love FC wameona giza baada ya kubugizwa magoli 6-1 na Kahawa Queens kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza iliyopigiwa Uwanja wa Chuo cha walimu cha Thogoto, Kikuyu.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Kahawa ikitafuta mabao ya mapema lakini wapi mlinda lango wa Joy Love, Khasandi Sharon alikuwa nga’ang’ari ndani ya dakika 27 ambapo alifanikiwa kuokoa zaidi ya mikwaju kumi. Dakika ya 28, Kahawa ya kocha, Joseph Wambua Mwanza ilipata goli la kufungua ukurasa lililofumwa kimiani na Jentrix Kuyudi.

Kahawa chini ya nahodha, Awuor Dorcas ilipata mabao mengine kupitia Patricia Amaase, Neddy Atieno, Emily Juma, Lucy Mukhwana na Everline ‘Etoo’ Juma na kufikisha alama 36 baada ya kushinda mechi zote 12 ambazo imeshiriki kwenye kipute hicho msimu huu.

Wafuasi wa Kahawa Queens wakiendelea kuwashangilia wachezaji hao wakicheza na Joy Love kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza katika uwanja wa Chuo cha walimu cha Thogoto, Kikuyu. Kahawa ilishinda magoli 6-1. Picha/ John Kimwere

”Nashukuru wenzangu kwa kuonyesha mchezo safi na kutimiza azimio letu la kubeba alama zote muhimu,” nahodha huyo alisema na kuongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo huo ili kumaliza ratiba ya ngarambe hiyo bila kuyeyusha alama yoyote. Kahawa inasubiria kutawazwa malkia wa kipute baada ya kuthibitishwa mabingwa ikiwa imebakisha mechi tatu.

Nayo Soccer Sisters ilikubali kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Mukuru Talent Academy huku Sunderland Samba FC ikilazimishwa kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Limuru Starlets.