Michezo

Kahawa Queens yaibuka moto wa kuotea mbali

June 10th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kahawa Queens iliandikisha ushindi wa pointi sita muhimu baada ya kucheza patashika mbili na kutua kileleni mwa mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Vipusa hao chini kocha, Joseph Wambua walibugiza Limuru Starlets kwa mabao 7-0 kisha waliizaba Sunderland Samba mabao 3-1 kwenye mechi iliyozua vurumai dakika za mwisho Uwanjani KNH, Nairobi.

Kahawa Queens ilijipatia ufanisi wa mechi zote mbili kupitia nahodha, Neddy Atieno aliyepiga ‘Hat trick,’ nao Emily Auma na Lucy Mukhwana kila mmoja alipiga mbili safi huku Jentrix Kuyudi, Joan Naututu na Judith Nafula kila mmoja akiitingia bao moja.

Naye Lorna Nyarinda aliifungia Sunderland Samba bao la kufuta machozi. Kahawa Queens ambayo ndiyo mwanzo wa ngoma kushiriki michuano ya kipute hicho ilivuna mafanikio hayo baada ya kukung’uta Moving The Goalpost (MTG) kwa mabao 3-0 wiki iliyopita.

”Nashukuru wachezaji wangu ingawa hatuna shangwe kufuatia vurumai zilizozuka dakika chache kabla ya mechi kukamilika,” kocha wa Kahawa Queens alisema.

Matokeo hayo yamefanya Kahawa Queens kutwaa uongozi wa ngarambe hiyo kwa alama 15, tatu mbele ya Sunderland Samba baada ya kucheza mechi tano na saba mtawalia.

Nayo MTG inafunga tatu bora kwa kufikisha alama kumi sawa na Mukuru Talent Academy pia Mombasa Olympic kwa usajari huo tofauti ikiwa idadi ya mabao.