Michezo

Kahawa United wafuzu kucheza na wakali wa soka

May 20th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Kahawa United imepandishwa ngazi kushiriki mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza, baada ya kurarua JAYSA FC mabao 5-0 kwenye mchuano wa fainali uliyopigiwa Kenyatta Stadium, mjini Machakos.

Kipindi cha kwanza vipusa hao walitoka nguvu sawa baada ya kushuka dimbani bila huduma za kati ya wachezaji mahiri Neddy Atieno (nahodha) na Everline Juma.

Kipindi cha lala salama Kahawa United ilionekana kurejea kivingine baada ya kocha wake, Joseph Wambua kuwaingiza uwanjani wachezaji hao wawili na kuwatoa Lillian Ngina pia Lucy Mukhwana.

Nguvu mpya hao walizindua wenzao kwenye patashika hiyo huku Neddy Atieno alifaulu kupiga ‘hat trick’, nao Magaret Atieno na Patricia Amaase kila mmoja akiitingia bao moja.

“Tayari tumeanza kupiga shughuli zetu vizuri maana tumepania kupigana kwa udi na uvumba kusaka tikiti ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi Kuu nchini (KWPL) msimu ujao,” nahodha wa Kahawa United alisema.

Kocha wa Kahawa United alipongeza kikosi chake kwa kujituma kiume na kuhakikisha kimetimiza azimio la kusonga mbele.

Kahawa United ilishiriki fainali hiyo baada ya kuibuka malkia wa Nairobi womens Regional League (NWRL) msimu uliyopita.

Kikosi hicho kilitawazwa malkia wa taji hilo kilipobeba mabao 3-0 mbele ya uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.